
KAIMU Mkuu wa Utawala wa JKT, Kanali Juma Mrai, akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 27,2025katika Mako Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kuhusu wito wa vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kwa mwaka 2025 kujiunga na mafunzo ya JKT.
Na.Alex Sonna-DODOMA
JESHI la Kujenga Taifa (JKT), linawaita vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kwa mwaka 2025 kutoka shule zote za Tanzania bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2025.
Hayo yamesemwa leo Mei 27, 2025 na Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT, Kanali Juma Mrai, amefafanua kuwa pamoja na wito huo, JKT limewapangia makambi watakao kwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Mei 28 hadi Juni 8,2025.
Kanali Mrai amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana kujengewa uzalendo, umoja wa kitaifa, kufundishwa stadi za kazi na maisha pamoja na utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa.
Kanali Mrai amesema vijana hao wamepangwa katika kambi tofauti ikiwemo kambi za JKT Rwamkoma - Mara, JKT Msange - Tabora, JKT Ruvu - Pwani, JKT Mpwapwa, Makutupora JKT - Dodoma, JKT Mafinga - Iringa, JKT Mlale - Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba - Tanga, JKT Makuyuni - Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila - Kigoma, JKT Itaka - Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa - Rukwa, JKT Nachingwea - Lindi, JKT Kibiti- Pwani pamoja na Oljoro JKT- Arusha.
Aidha Kanali Mrai amesema kuwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wanapaswa kuripoti katika kambi ya Ruvu JKT Mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.
Hata hivyo JKT linawataka vijana hao kuripoti wakiwa na Bukta ya Dark Bluu yenye mpira kiunoni(lastic)iliyo na mfuko mmoja nyuma,urefu unaoishia magotini,isiyo na zipu, T-shirt rangi ya kijani,Raba za Michezo zenye rangi ya kijani na Bluu,shuka mbili za kulalia zenye rangi ya Bluu bahari,soksi ndefu za rangi nyeusi,Nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi,Track suit ya rangi ya kijani au Bluu,Nyaraka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu,zikiwemo Cheti Cha kuzaliwa,vyeti vya kuhitimu kidato Cha Nne,nauli ya kwenda kuripoti makambini na kurudi nyumbani.
"Orodha kamili ya majina ya vijana hao,Makambi ya JKT waliopangiwa na maeneo makambi hayo yalipo na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo,inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.mil.tz"
Aidha ili kufahamu Kambi kijana aliyopangiwa,atatakiwa kuingiza jina la Shule au namba ya Shule aliyohitimu elimu ya kidato Cha Sita,mbele ya jina lake la Shule ataona neno lililoandika waliochaguliwa,akichagua neno hilo ataona jina au majina ya waliochaguliwa kujiunga na Mafunzo ya JKT Kwa Mujibu wa sheria kwa mwaka 2025,ikionesha kambi aliyopangiwa,Mkoa na wilaya ilipo kambi hiyo.
"Ili kuona majina yote ya vijana na Kambi waliopangiwa,mtumiaji atapakua JKT PDF 2025 iliyopo juu kulia katika ukurasa huo" Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele anawakaribisha Vijana wote waliohitimu kidato Cha Sita mwaka 2025 kuungana na Vijana wenzao ili kujengewa uzalendo,Umoja wa Kitaifa,kufundishwa stadi za kazi,stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa lao
Post a Comment