Na Mapuli Kitina Misalaba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kudhibiti kiasi cha shilingi milioni 92.16 ambazo
zilikuwa zimefujwa na viongozi wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa
Tumbaku Ibambala (Ibambala AMCOS) katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa
Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akizungumza na waandishi wa
habari ambapo amesema fedha hizo zilipaswa kulipwa kwa wakulima waliopata
hasara kubwa kutokana na mafuriko yaliyoathiri uzalishaji wa zao la tumbaku
katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024. Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa
badala ya wakulima kulipwa, fedha hizo zilielekezwa kwenye akaunti binafsi za
viongozi wa chama hicho.
Watuhumiwa wa ubadhirifu huo ni Katibu Meneja wa
chama Bw. Charles Alex Shiyengo, Mwenyekiti Bw. Faida Paulo Deda, mke wa katibu
meneja Bi. Lucy Masanja Gidabita na mtoto wa katibu meneja Bw. Charles Charles
Masanja. Kwa pamoja waligawana shilingi milioni 151.53, huku wakulima 152
wakipewa kiasi kidogo cha shilingi milioni 11.62 pekee.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, Mwenyekiti Bw. Faida Paulo
Deda alijilipa TZS 53,066,743.54, Katibu Meneja Bw. Charles Shiyengo alijilipa
TZS 58,300,000/=. Bi. Lucy Masanja alipokea TZS 34,580,000.27, huku mtoto wao
akilipwa TZS 5,583,519.20.
Aidha, TAKUKURU imesema watu hao ni wanachama wa
chama hicho lakini walihamishiwa fedha hizo kwenye akaunti zao binafsi kinyume
na taratibu za maadili ya uongozi wa vyama vya ushirika.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU imeeleza kuwa
imeendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi tisa (9) yenye thamani ya TZS
2,056,092,213/= ambapo ushauri ulitolewa kurekebisha mapungufu yaliyobainika.
Kupitia shughuli za uelimishaji umma, TAKUKURU
imeimarisha klabu 61 za wapinga rushwa, kufanikisha mikutano ya hadhara 30,
semina 9, vipindi vya redio 5 na maonesho matatu (3). Katika wiki ya sheria,
wananchi 325 walipata elimu kupitia mabanda ya TAKUKURU.
Katika utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU Rafiki,
jumla ya vikao 14 vya kutatua kero vilifanyika na kupokea kero 55, ambapo 36
kati ya hizo zilitatuliwa.
Kuhusu uchunguzi, TAKUKURU imepokea malalamiko 52,
ambapo 20 yalihusiana moja kwa moja na rushwa. Kwa sasa kuna kesi 13
zinazoendelea mahakamani, ikiwemo kesi mpya 5, ambapo kesi mbili (2)
zimeshaamuliwa na washitakiwa kupatikana na hatia.
Kessy,
amewataka wananchi kushirikiana na taasisi hiyo kwa kuwafichua viongozi wala
rushwa, huku akisisitiza kuwa "Kuzuia rushwa ni jukumu letu
sote."
Post a Comment