SHINYANGA WENYEJI MAADHIMISHO SIKU YA MKUNGA DUNIANI KITAIFA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MAADHIMISHO ya Siku ya Mkunga Duniani Kitaifa yanafanyika mkoani Shinyanga, huku Mgeni Rasmi akiwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk.Seif Shekalaghe.
Maadhimisho hayo yameanza leo Mei 4,2025 na yatahitimishwa kesho Mei 5 na yanafanyika katika Viwanja vya Zimamoto Mjini Shinyanga.
Rais wa Chama Cha Wakunga wa Tanzania (TAMA)Dk. Beatrice Mwilike, akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa maadhimisho hayo mwaka huu wameamua kuyafanyia mkoani Shinyanga, ili kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi juu ya masuala ya afya ya uzazi, na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Maadhimisho ya siku ya ukunga duniani kitaifa hapa nchini Tanzania, mwaka huu tumeamua kuyafanyia hapa mkoani Shinyanga,na Mgeni Rasmi atakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk.Seif Shekalaghe,”amesema Dk Mwilike.
Aidha,amesema katika maadhimisho hayo, elimu mbalimbali zitatolewa bure kwa wananchi, yakiwamo masuala ya afya ya uzazi,pia kutakuwa na huduma ya utoaji wa damu salama ili kuchangia benki ya damu,na hata kuokoa wazazi wakati wa kujifungua.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo,wajitokeze kwa wingi kwenye maadhimisho hayo ya siku ya ukunga dunian mkoani humo ili wapate elimu mbalimbali bure za masuala ya afya na afya ya uzazi.
Kauli Mbiu katika maadhimisho ya siku ya ukunga duniani mwaka huu inasema”Mkunga ni Nguzo Muhimu katika kila Janga.”
Post a Comment