
KUMEKUCHA: Msajili Asitisha Ruzuku ya Chadema
Msajili wa Vyama vya siasa nchini Tanzania kulingana na Mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 18(6) cha sheria ya Vyama vya siasa, ametangaza Jumanne Mei 27, 2025 kusitisha kutoa ruzuku kwa Chama Cha Demokrasia na maendeleo Chadema hadi pale watakapotekeleza maelekezo ya Ofisi ya Msajili kutokana na Chadema kutokuwa na Viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha hizo za Umma.
Hatua ya Ofisi ya msajili wa Vyama vya siasa imefikiwa mara baada ya kueleza kuwa Chadema imekaidi mara kadhaa maamuzi ya Ofisi ya msajili, ikiwemo taarifa ya Mei 25, 2025, ambapo Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche akisoma Maazimio ya Kamati kuu ya Chama, alieleza kuwa maamuzi na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya siasa kuhusu malalamiko ya Bw. Lembrus Mchome ni batili na hawatoyafanyia kazi.
Aidha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa imeendelea kusisitiza kuwa Bw. John Mnyika, Amani Golugwa, Ali Ibrahim Juma, Godbless Lema, Dkt. Rugemeleza Nshala, Rose Mayemba, Salima Kasanzu na Hafidhi Ali Salehe sio viongozi wa Chadema sambamba na watendaji wengine wote walioteuliwa katika Kikao cha Baraza kuu la Januari 2025.
Taarifa ya Msajili wa Vyama vya siasa iliyochapishwa na kusainiwa na Abuu Kimario, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na elimu ya Uraia, imewasihi pia wananchi, wadau na mamlaka na taasisi za serikali na binafsi kutowapa ushirikiano na huduma wanachama walioorodheshwa hapo juu, endapo watakuwa wakihitaji huduma fulani kama Viongozi wa Chadema, ambapo imeelezwa kuwa Viongozi halali wa Vyama vya siasa ni wale tu wanaotambuliwa na Msajili wa Vyama vya siasa nchini.
Msajili huyo pia amebainisha kwamba endapo Chadema wataendelea kukaidi kutekeleza maamuzi na maelekezo waliyopatiwa basi Mamlaka husika zitatakiwa kuchukua hatua za kisheria na kijinai pamoja na kuwasimamisha wanaojifanya kuwa Vionglzi wa Chadema katika kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa Kifungu cha 21E cha sheria ya Vyama vya siasa nchini.
Msajili pia amekumbusha kwamba kwa mujibu wa sheria anayo mamlaka ya kusimamisha usajili wa Chadema endapo kitaendelea kuwatambua wanaojiita Viongozi wa Chama hicho.
Post a Comment