
Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amethibitisha rasmi kukamilika kwa zoezi la uokoaji kufuatia ajali ya kifusi katika Mgodi wa Dhahabu wa Mwakitolyo, unaomilikiwa na Kikundi cha Wachimbaji cha HAPA KAZI TU, iliyotokea Jumamosi ya Mei 17, 2025.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mtatiro amesema kuwa jumla ya watu 17 walihusika kwenye ajali hiyo ambapo 11 waliokolewa wakiwa hai na 6 walipoteza maisha. Amesisitiza kuwa zoezi la uokoaji limekamilika kwa mafanikio na hakuna mtu mwingine aliyebaki kifusini.
"Tulitumia mashine za kisasa zaidi ya 10, lakini 4 tu zilitosha kufanya kazi yote ya uokoaji. Tulihamisha kifusi chote, tukakichambua kwa mashine na kwa mikono, na hakuna mtu mwingine aliyebakia ndani," amesema DC Mtatiro.
Aidha, amesema kuwa hakuna taarifa yoyote ya mtu kupotea kutoka katika jamii ya Mwakitolyo au Shinyanga kwa ujumla, na familia zote zimethibitisha kutokuwepo kwa mtu mwingine aliyepotea zaidi ya wale 17 waliotambuliwa.
"Majeruhi walioko hospitalini waliweka wazi kuwa wakati wa ajali walikuwa watu 17 tu, na wanajuana vizuri. Taarifa nyingine zinazodai kuwa kuna watu wameachwa chini ya kifusi siyo sahihi, ni za kupotosha na zinapaswa kupuuzwa," ameongeza Mtatiro.
Ajali hiyo iliyotokea katika eneo la wazi lenye nafasi kubwa kwa mashine kufanya kazi kwa ufanisi, ilihusisha juhudi za pamoja za serikali, wananchi, na mashine maalum za migodi, jambo lililowezesha uokoaji kufanyika kwa weledi na kasi.
Taarifa hii inathibitisha kuwa operesheni hiyo imehitimishwa rasmi, na taharuki yoyote inayosambazwa bila uthibitisho imetajwa kuwa haina msingi wowote.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro akizungumza.
Post a Comment