" PSSSF YATAJA MAFANIKIO MAKUBWA NDANI YA MIAKA 7, YAAHIDI KUSHIRIKIANO NA MISA TANZANIA KATIKA UTOAJI TAARIFA ZA MAFAO

PSSSF YATAJA MAFANIKIO MAKUBWA NDANI YA MIAKA 7, YAAHIDI KUSHIRIKIANO NA MISA TANZANIA KATIKA UTOAJI TAARIFA ZA MAFAO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeeleza kuwa katika kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa kwake, umeendelea kuboresha huduma kwa wanachama wake kwa kutumia mifumo ya kisasa inayowawezesha kupata mafao kwa urahisi na bila usumbufu.

Akizungumza kwenye mkutano kati ya PSSSF na wanachama wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Tanzania (MISA Tanzania), Meneja wa Mafao wa PSSSF, Ramadhani Mkenyenge, amesema Serikali kupitia Sheria Namba 2 ya mwaka 2018 iliunganisha mifuko ya LAPF, PSPF, GEPF na PPF na kuunda PSSSF, ili kuimarisha ufanisi na usimamizi wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma.

Ameeleza kuwa tangu Agosti 1, 2018 wanachama wa mifuko hiyo waliokuwa watumishi wa umma walihamishiwa PSSSF, huku waliokuwa sekta binafsi wakihamishiwa NSSF na kwamba  kuanzia Februari 2019 watumishi wa umma waliokuwa kwenye NSSF walihamishiwa PSSSF.

Mkenyenge amebainisha kuwa mfuko huo ulianza na wanachama hai 862,986 na hadi kufikia Juni 30, 2025 una jumla ya wanachama hai 807,010 huku akisisitiza kuwa katika kipindi hicho, PSSSF imejipambanua kwa kutekeleza malipo ya mafao kwa uwazi na kasi kupitia mifumo ya kielektroniki inayounganishwa na taarifa za wanachama, hatua iliyopunguza ucheleweshaji na gharama za kufuatilia mafao.

“Tunachofanya sasa ni kuhakikisha mwanachama anapata stahiki zake bila kulazimika kusafiri mara nyingi au kupanga foleni. Mfumo wetu unaruhusu malipo kuidhinishwa na kukamilika kwa haraka pindi taratibu zote zinapokamilika,” amesema Mkenyenge.

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, PSSSF inalenga kukusanya wastani wa shilingi bilioni 168.25 kwa mwezi, ongezeko la asilimia 43.42 kutoka bilioni 117.31 zilizokusanywa kwa mwezi katika mwaka uliopita.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema ushirikiano kati ya PSSSF na vyombo vya habari ni muhimu ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu mafao na huduma za mfuko huo. “Waandishi wa habari ni kiungo cha moja kwa moja kati ya taasisi na wananchi, hivyo kushirikiana nao ni kuongeza nguvu ya kuwafikia wanufaika,” amesema Soko.

Mkutano huo umehitimishwa kwa makubaliano ya kuendelea kuimarisha elimu kwa umma kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, sambamba na kuongeza ushirikiano katika uhamasishaji wa wanachama wapya na kuimarisha uelewa kuhusu haki na wajibu wao.

PSSSF, yenye kauli mbiu ya “Leo. Kesho. Pamoja.”, inatoa mafao ya muda mrefu na muda mfupi, yakiwemo mafao ya uzeeni, ulemavu, kifo, utegemezi, kukosa ajira, ugonjwa na uzazi, huku ikitekeleza dira yake ya kuwa mfuko unaotoa huduma bora zaidi za hifadhi ya jamii nchini.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post