Dar es Salaam. Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), imeendelea kuonesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, baada ya kukusanya Sh749 bilioni hadi kufikia Mei 7, 2025 — sawa na asilimia 67 ya lengo la mwaka wa fedha 2024/25 la Sh1.113 trilioni.
Taarifa hiyo ilitolewa Jumatano, May 7, 2025 na Bi. Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya mashirika ya kibiashara kutoka OMH.
Bi. Mauki alikuwa anazungumza kuelekea Siku ya Gawio ‘Gawio Day’ itakayoadhimishwa Juni 6, 2025, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kupokea gawio kutoka taasisi mbalimbali za umma.
Akizungumza hapo awali, Jumanne usiku, katika kipindi maalumu cha dakika 30 cha TBC, Bi. Mauki alisema taasisi nyingi bado zinaendelea na mikutano yao ya wanahisa (AGMs), hivyo OMH ina uhakika wa kufikia lengo la mwaka.
Maudhui ya kipindi hicho cha TBC yalilenga kuonesha mchango wa mashirika na taasisi za umma katika maendeleo ya Taifa.
“Ni imani yetu tutampatia gawio nono Mheshimiwa Rais mwezi Juni 6,” alisema kwa kujiamini.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya Sh749 bilioni zilizokusanywa hadi Mei 7, gawio kutoka kwa mashirika ya umma na Kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache limechangia asilimia 63 ya mapato hayo, huku mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi unaokwenda moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ukichangia asilimia 29.
Mapato mengineyo, yakiwemo Marejesho ya mikopo na riba (onlending), na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa TTMS, yamechangia asilimia 8 ya jumla hiyo.
Kiasi ambacho kimekusanywa hadi kufikia Mei 7 mwaka huu ni kikubwa ukilinganisha na mwaka uliopita kipindi kama hiki, ambapo makusanyo yalikuwa Sh500 bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.
Siri ya mafanikio
Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu amesema kuwa mafanikio ya OMH yanatokana na utekelezaji wa mikakati ya usimamizi iliyowekwa na ofisi hiyo.
Alisema ofisi yake imekuwa ikifanya mapaitio ya mikataba ya wanahisa, mikataba ya uendeshaji pamoja na mikataba ya kiufundi ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza gawio la Serikali.
Aliongeza kuwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA, hasa mfumo wa Serikali wa kukusanya mapato kielektroniki (GePG), yameongeza uwazi, weledi na kasi ya ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza Alhamis Asubuhi wakati wa kipindi maalumu cha Kumepambazuka cha Redio One, Bi. Neema Musomba, Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema uchambuzi wa taarifa za utendaji wa taasisi kila robo mwaka, nusu mwaka na mwisho wa mwaka, pamoja na uhakiki wa bajeti kabla ya kuidhinishwa, umewezesha serikali kuwa na udhibiti wa karibu zaidi wa mwenendo wa kifedha wa mashirika hayo.
Kwa upande mwingine, alibainisha kuwa tathmini za usimamizi wa utekelezaji wa mikataba kati ya Msajili wa Hazina na Wenyeviti wa Bodi za mashirika zimeimarika, jambo lililoleta uwajibikaji wa moja kwa moja kwa viongozi wa taasisi hizo.
Mapato yasiyo ya kodi: Nguzo ya maendeleo ya Taifa
Mapato yasiyo ya kodi yameendelea kuwa mhimili wa kugharamia huduma za msingi kama elimu, afya, maji safi na miundombinu.
Kupitia makusanyo haya, serikali imepunguza utegemezi wake kwa misaada ya wahisani na mikopo kutoka nje ya nchi, hali inayochochea uhuru wa kiuchumi na sera.
“Mapato hayo huchochea uwajibikaji wa mashirika ya umma, huongeza ufanisi wa utendaji kazi, na hujenga imani ya wananchi kwa taasisi za umma,” alisema Bi. Musomba
“Gawio si tu fedha – ni ishara ya utendaji bora, uwajibikaji, na ushiriki wa taasisi katika maendeleo ya Taifa.”
OMH imeelekeza taasisi zote ambazo bado hazijawasilisha gawio la mwaka huu kuhakikisha zimefanya hivyo kabla ya tarehe 30 Juni, 2025, ili kusaidia kufanikisha mipango ya serikali kwa mwaka wa fedha unaoendelea.
Post a Comment