
Martha Karua wa Kenya Amjibu Rais wa Tanzania Kurudishwa Kenya
Mwanasiasa wa chama cha People Liberation Party (PLP), Martha Karua, amemjibu moja kwa moja Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kufuatia kuzuiwa kwake kushiriki katika kesi ya kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu.
Karua alikuwa amesafiri pamoja na viongozi wengine wa kisiasa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kwa lengo la kushuhudia mwenendo wa kesi ya Lissu, lakini walizuiwa mpakani mwa Tanzania na baadaye kufurushwa.
Rais Suluhu alidai kwamba ujio wa kundi hilo ulikuwa wa kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake, kauli ambayo Karua ameikataa vikali. Kupitia ujumbe aliouweka kwenye X (zamani Twitter), Karua alisema kuwa waliingia nchini humo kwa mujibu wa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kufurushwa kwao hakukuwa halali.
“Hatukuvamia nchi ya Tanzania @SuluhuSamia, tulikuja kihalali kama wanajumuiya, tukazuiliwa kinyume cha mkataba wa @jumuiya na kufurushwa inje,” aliandika Karua.

Kauli hiyo ya Karua imeibua mjadala mpana kuhusu uhuru wa kusafiri na kushiriki katika shughuli za kidemokrasia ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Karua alisisitiza kuwa safari yao haikuwa ya fujo, bali ilikuwa ya mshikamano wa kidemokrasia na kwamba haki ya wananchi wa jumuiya hiyo kutembea na kushiriki shughuli ndani ya nchi wanachama lazima iheshimiwe.
Hadi sasa, serikali ya Tanzania haijatoa tamko rasmi kuhusu kufurushwa kwa viongozi hao, huku serikali ya Kenya pia ikiwa haijazungumzia suala hilo.
Wachambuzi wa siasa na mashirika ya kijamii wameelezea hofu yao kuwa tukio hilo ni dalili ya kupungua kwa nafasi ya demokrasia katika ukanda huo, na wameitaka Sekretarieti ya EAC kutoa mwongozo wa wazi kuhusu haki za wananchi ndani ya jumuiya.
Licha ya tukio hilo, Karua amesisitiza kuwa ataendelea kutetea misingi ya haki, uwazi na mshikamano wa kikanda.
Post a Comment