" KUKAMILIKA KWA MIRADI YA KIMKAKATI KANDA YA ZIWA KUTOA MSUKUMO MPYA KATIKA UCHUMI – MSIGWA

KUKAMILIKA KWA MIRADI YA KIMKAKATI KANDA YA ZIWA KUTOA MSUKUMO MPYA KATIKA UCHUMI – MSIGWA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kukamilika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ametoa kauli hiyo  Mei 2, 2025, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa Jijini Mwanza, ambapo amepongeza hatua nzuri zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo huku akitoa wito kwa wakandarasi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia muda.

Katika ziara hiyo, Msigwa ametembelea na kukagua miradi mitatu muhimu ambayo ni: ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza, daraja la Busisi-kigongo ambalo limefikia asilimia 99 ya ujenzi, pamoja na ujenzi wa vivuko vipya vitano vinavyojengwa katika yadi ya Songoro Marine Transport Limited jijini Mwanza.

Miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa ukanda wa Ziwa Victoria ni ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza, unaotekelezwa kwa ubia kati ya kampuni za Gas Entec na Kangnam Corporation zote kutoka Korea Kusini kwa kushirikiana na SUMA JKT ya Tanzania.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Januari 17, 2019 na hadi sasa umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake. Gharama za mradi zinakadiriwa kufikia Dola za Kimarekani 51,830,440.28 sawa na Shilingi Bilioni 138.9. Hadi sasa Serikali tayari imelipa Dola za Kimarekani 48,899,790.26 (asilimia 94.35 ya gharama zote), sawa na Shilingi Bilioni 131.1.

Meli hiyo itakapokamilika, itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo ya tani 400, magari madogo 20 na malori matatu. Itakuwa na madaraja sita ya abiria: Economy (abiria 834), Business Class (200), Second Sleeping (100), First Class (60), Executive (4) na VIP Class (2).

Meli hiyo itafanya safari kati ya Mwanza, Bukoba, Musoma kupitia Kemondo Bay pamoja na nchi jirani za Uganda na Kenya, hivyo kuimarisha biashara, usafirishaji na mahusiano ya kikanda.

Kwa sasa kazi iliyosalia ni ufungaji wa viti na samani, ambapo kontena tisa za viti tayari zimeshawasili na mzigo wa mwisho wa samani za vyumba vya kulala unatarajiwa kuwasili katikati ya mwezi Mei.

Wizara kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa vivuko vipya vitano pamoja na ukarabati wa vivuko vitatu katika Kanda ya Ziwa.

Mradi huo unatekelezwa na Songoro Marine Transport Limited ya jijini Mwanza na unalenga kutoa huduma katika maeneo ya Bwiro – Bukondo (Ukerewe), Ijinga – Kahangala (Magu), Kisorya – Rugezi (Ukerewe), Nyakaliro – Kome (Sengerema) na Buyagu – Mbalika (Sengerema/Misungwi).

Gharama za utekelezaji wa miradi hii ni Shilingi Bilioni 18.6 pamoja na Dola za Kimarekani Milioni 3.79. Hadi sasa Serikali imelipa kiasi cha Shilingi Bilioni 21.7 sawa na asilimia 75 ya madai ya mkandarasi.

Usimamizi wa miradi hiyo unafanywa na Mtaalam Mshauri kutoka DMI pamoja na udhibiti wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), ili kuhakikisha ubora na viwango vinazingatiwa kikamilifu.

Katika hatua nyingine, daraja la Busisi-kigongo limefikia asilimia 99 ya ujenzi. Daraja hilo linatarajiwa kuwa kiungo muhimu kati ya mikoa ya Mwanza na Geita, na hivyo kupunguza utegemezi wa vivuko na kuboresha mzunguko wa shughuli za kiuchumi kati ya mikoa hiyo.

Msigwa amewataka wakandarasi kote nchini kuendelea kutekeleza miradi kwa ubora na kwa muda uliopangwa, huku akiwakumbusha wananchi kulinda miradi hiyo mara baada ya kukamilika.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wakandarasi wanaotekeleza miradi kwa weledi. Lakini pia, wananchi tunapaswa kuitunza miundombinu hii kwa sababu ni ya kwetu wote,” amesema Msingwa.

Ameongeza kuwa uwepo wa miradi hiyo utasaidia kuchochea mzunguko wa fedha, kupunguza gharama za usafiri, na kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta kama utalii, biashara, na usafirishaji katika maeneo yote ya Ziwa Victoria.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Msigwa aliambatana na waandishi wa habari kutoka Shinyanga na Mwanza ambao wameeleza kufurahishwa na hatua za utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kuendelea kuripoti kwa weledi baada ya kujionea maendeleo kwa macho yao.

Ziara ya Katibu Mkuu huyo imehitimishwa jijini Mwanza Mei 2, 2025, ambapo anatarajiwa kuendelea na ziara yake Mkoani Shinyanga leo Mei 3, 2025.













Post a Comment

Previous Post Next Post