" NICK LUHENDE AMWANDIKIA BARUA YA WAZI AMOS MAKALLA: "SHINYANGA HAIHITAJI MANENO MATAMU, INAHITAJI MAJIBU YA KWELI"

NICK LUHENDE AMWANDIKIA BARUA YA WAZI AMOS MAKALLA: "SHINYANGA HAIHITAJI MANENO MATAMU, INAHITAJI MAJIBU YA KWELI"

 

BARUA YA WAZI KWA MWENEZI WA CCM TAIFA – MGENI JIMBONI SHINYANGA

Ndugu Mwenezi,
Heshima yako.

*YAH: MAENDELEO YA SHINYANGA MJINI YANAHITAJI MAJIBU YA KWELI – SI MANENO MATAMU PEKEE*

Nimepokea kwa hisia mchanganyiko taarifa ya ujio wako katika jimbo letu. Kama Mtanzania mzalendo, ninaheshimu nafasi yako kama msemaji wa chama, lakini pia nina wajibu wa kusema kile ambacho wananchi wa kawaida tunahisi, kuona, na kupitia kila siku.

Mara nyingi mnapotembelea maeneo kama haya, huambatana na maneno ya sifa kwa serikali ya awamu ya sita – kuhusu fedha zilizomwagwa, miradi iliyotekelezwa, na ahadi zilizo mbele yetu.
Lakini kwa upande wa Jimbo la Shinyanga Mjini, ukweli ni kuwa hali yetu haileti picha hiyo mnavyoichora. Tuna changamoto kubwa na za muda mrefu – ambazo hazifai kufunikwa kwa maneno ya kisiasa.

*Sekta ya Kilimo na Uchumi:*
Wakulima wetu wa pamba, dhahabu nyeupe ya mkoa huu, bado wanaishi kwa tabu. Bei ni ndogo (msimu huu kilo itauzwa kwa Tshs 1,150), miundombinu ya masoko ni mibovu, na hakuna viwanda vya kutupa thamani zaidi. Hali hii inaendelea kuzorota, kama inavyooneshwa na hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo iliyowasilishwa tarehe 21 Mei 2025, ambapo imetajwa kuwa kwa mwaka 2024/25, uzalishaji wa pamba umeshuka hadi tani 149,361 – sawa na asilimia 29 tu ya lengo la uzalishaji. Hii ni karibu nusu ya kiwango cha mwaka uliotangulia (tani 282,510 kwa 2023/24). Takwimu hizi zinaakisi anguko la moja kwa moja la kipato kwa maelfu ya wakulima wa maeneo kama Shinyanga. Leo hii hatuna shughuli ya kiuchumi ya uhakika inayotambulisha Jimbo hili.

*Sekta ya Afya:*
Hospitali yetu ya Rufaa ya Mwawaza ilitajwa kwenye ripoti ya CAG ya mwaka jana kuwa na dawa zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1 zilizokuwa zimepitwa na wakati na kutakiwa kuteketezwa. Ripoti ya mwaka huu inaonesha hospitali hiyo imepokea chini ya nusu ya mahitaji ya dawa kutoka MSD. Hili linaumiza wananchi – hasa maskini wasio na uwezo wa kununua dawa binafsi.

*Elimu:*
Matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne waliomaliza mwaka 2022 yanaonesha asilimia 58 wamepata division four na zero. Hii ni tahadhari kwamba kizazi kijacho kinapotea. Tunahitaji mpango madhubuti – siyo ziara za maneno pekee. Hili ni aibu kwa eneo lililojaa vijana na Mbunge wake akiwa ni Naibu Waziri mwenye dhamana ya vijana hao.

*Miundombinu na Uwekezaji:*
Barabara za ndani ya mji zinasikitisha. Soko kuu lina mkwamo. Hatuna kivutio kikubwa cha wawekezaji, na hali ya mazingira ya biashara bado ni dhaifu.

Ndugu, tunataka kusikia mkakati mahsusi kwa ajili ya afya zetu, elimu ya watoto wetu, uchumi wa wakulima wetu, na miundombinu ya mji wetu. Na tunataka hayo yatekelezwe – siyo tu kusikika vizuri kwenye majukwaa.

Na zaidi ya yote, endapo utatimiza wajibu wako kwa kusema ukweli, kusikiliza vilio vya wananchi, na kuwasilisha ujumbe sahihi kwa uongozi wa juu wa chama, basi *utakuwa umefanya kazi kubwa ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kueleweka kwa wanaShinyanga* – si kwa sifa pekee bali kwa hatua na mabadiliko ya kweli.

Ninaandika haya nikiwa raia mwenye mapenzi ya kweli kwa jimbo na nchi yangu. Tufahamu tu mustakabali wa kweli wa Shinyanga Mjini – mji ambao umekuwa ukiteseka kimya kimya kwa miaka mingi.

Wasalaam,
Nick Luhende
Raia Mwandamizi
22 Mei 2025
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post