" POLISI MBEYA YAKAMATA WANNE KWA TUHUMA ZA UHUJUMU MIRADI YA MAJI

POLISI MBEYA YAKAMATA WANNE KWA TUHUMA ZA UHUJUMU MIRADI YA MAJI

 

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kuhujumu mradi wa kimkakati wa maji wa miji 28, baada ya kuiba mabomba 50 ya chuma pamoja na mashine ya kupimia usawa wa ardhi (levelling machine) na stendi yake — vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa mradi huo mkubwa wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamini Kuzaga, alisema watuhumiwa hao walikamatwa kati ya tarehe 22 Aprili na 15 Mei, 2025, katika misako mbalimbali iliyofanyika maeneo tofauti ya Mkoa wa Mbeya.

“Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni kuhakikisha wote waliohusika na uhalifu huu wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Kamanda Kuzaga.

Katika tukio tofauti, Jeshi hilo linamshikilia Hassan Twailam Hassan (40), mkazi wa Tanga, kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 25, zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye mabunda sita ya Nylon.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Mei 8, 2025, katika kizuizi cha Polisi kilichopo eneo la Mpakani, Wilaya ya Mbarali, kwenye barabara kuu ya Mbeya – Njombe. Alikuwa akisafirisha dawa hizo kwa kutumia basi la abiria lenye namba za usajili T.809 DXJ aina ya Yutong linalomilikiwa na kampuni ya Abood, akitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam. Alikuwa ameficha dawa hizo kwenye sanduku.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote waliobainika kuhusika na uhalifu huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post