" SHINYANGA: WATIA NIA 8 WA ACT WAZALENDO WAREJESHA FOMU ZA UBUNGE

SHINYANGA: WATIA NIA 8 WA ACT WAZALENDO WAREJESHA FOMU ZA UBUNGE

Na Mapuli Kitina Misalaba

Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea ubunge kupitia Chama cha ACT Wazalendo linaendelea kwa kasi mkoani Shinyanga, ambapo leo watia nia nane wamerejesha fomu kutoka majimbo ya Shinyanga Mjini, Itwangi na Kishapu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa wa Oganizesheni, Mafunzo na Uchaguzi ACT Wazalendo Taifa, Bwana Risasi Semasaba, amesema kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri katika majimbo yote na linatarajiwa kufungwa rasmi Mei 31, 2025.

Amesema hadi sasa katika Jimbo la Shinyanga Mjini pekee, watu watano tayari wamerejesha fomu, jambo linaloonesha mwitikio mzuri wa wanachama na wananchi walioguswa na ajenda za chama hicho.

Baadhi ya watia nia wamezungumza mara baada ya kurejesha fomu zao, wakieleza dhamira yao ya kuleta mabadiliko chanya endapo watapewa ridhaa ya kuipeperusha bendera ya chama hicho na hatimaye kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Zoezi hilo linaendelea katika ofisi za ACT Wazalendo mkoani humo huku viongozi wa chama hicho wakisisitiza kuwa mchakato huo unazingatia misingi ya uwazi, usawa na demokrasia.

 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post