Katika hatua muhimu ya kisiasa kimataifa, Mwanasiasa maarufu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa International Democrat Union (IDU), shirika linalojumuisha vyama vya kidemokrasia duniani. Taarifa rasmi ya chama hicho imeeleza kuwa uchaguzi huo umefanyika mjini Brussels, Ubelgiji, katika mkutano mkuu uliohusisha wajumbe kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CHADEMA kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Democracy Union of Africa (DUA) kanda ya Afrika Mashariki, Deogratias Munishi, ambapo wajumbe wa IDU walimchagua Waziri Mkuu wa zamani wa Canada, Stephen J. Harper, kuendelea na nafasi ya Mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo. Katika uchaguzi huo huo, jina la Lissu lilipendekezwa na kuungwa mkono kwa kauli moja kuwa Makamu Mwenyekiti wa IDU.
Uteuzi wa Tundu Lissu umeelezwa kuwa ni ushindi mkubwa si tu kwa CHADEMA bali pia kwa harakati za kidemokrasia barani Afrika, hasa ukizingatia mazingira ya kisiasa alikopitia. Lissu, ambaye aliwahi kulengwa kwa jaribio la kutolewa uhai mwaka 2017, ameendelea kuwa nembo ya mapambano ya haki za binadamu, utawala bora na uhuru wa kujieleza nchini Tanzania.
Wajumbe wa mkutano huo wamesisitiza kuwa uteuzi wa Lissu unadhihirisha jinsi jumuiya ya kimataifa inavyotambua mchango wake katika kulinda misingi ya demokrasia. Wameeleza kuwa historia na msimamo wa Lissu dhidi ya udikteta na ukiukwaji wa haki, kuliwapa imani ya kumuamini kama kiongozi anayeweza kuwakilisha sauti ya Afrika kwenye majukwaa ya kidemokrasia duniani.
Taarifa hiyo ilitolewa rasmi na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, tarehe 24 Mei 2025, ikiwa ni ushuhuda wa kuimarika kwa ushawishi wa chama hicho nje ya mipaka ya Tanzania. Hatua hiyo imepokelewa kwa heshima kubwa na wafuasi wa demokrasia, huku wengine wakitafsiri kama ishara ya matumaini kwa mustakabali wa kisiasa wa bara la Afrika.
Post a Comment