" UKATILI WA KIJINSIA WATIKISA KISHAPU – ZAIDI YA MATUKIO 500 YARIPOTIWA MWAKA 2024

UKATILI WA KIJINSIA WATIKISA KISHAPU – ZAIDI YA MATUKIO 500 YARIPOTIWA MWAKA 2024

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea kuwa chanzo kikuu cha mateso, vifo visivyo vya lazima, kukatishwa kwa ndoto za watoto wa kike, na kuzorota kwa haki za binadamu. Takwimu zilizotolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Ibrahim Sakulia, zinaonesha picha halisi ya uhalisia wa maisha ya wanawake na wasichana katika wilaya hiyo.

Kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024, jumla ya matukio 64 ya ubakaji na ulawiti yameripotiwa – wanawake wakiwa 61 na wanaume watatu. Idadi hiyo inazidi kuongezeka kwa kasi, kwani kati ya Aprili hadi Juni pekee, matukio ya ubakaji na ndoa za utotoni kwa jinsi ya kike yalifikia 203. Kuanzia Julai hadi Septemba, visa vya ukatili wa kingono viliripotiwa 89 kwa wanawake na tukio moja kwa mwanaume, huku kuanzia Oktoba hadi Desemba matukio yakiwa 157 kwa wanawake na mawili kwa wanaume.

Takwimu hizi zinaibua maswali mazito kuhusu usalama wa wanawake na wasichana katika jamii, na ni dhahiri kuwa kuna haja ya hatua za haraka na madhubuti ili kupunguza ukatili huu ambao umeonekana kuota mizizi.

Takwimu za kitaifa za mwaka 2022 zinaonesha kuwa asilimia 85 ya wanawake walihudhuria kliniki wakati wa kujifungua, huku asilimia 81 wakijifungulia katika vituo vya afya, na 65% wakisaidiwa na wahudumu wa afya. Hata hivyo, bado changamoto kubwa ipo kwenye uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu afya ya uzazi.

Kati ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49, ni asilimia 47 hadi 49.6 pekee waliofanya maamuzi ya kutumia njia za uzazi wa mpango au kujali afya zao pasipo kuingiliwa. Hali hii inaashiria kuwa bado wanaume wanashikilia maamuzi mengi kuhusu afya ya uzazi wa wenza wao, jambo linalohitaji mjadala wa wazi katika familia na jamii.

Katika viwango vya ukatili kwa mujibu wa viashiria vya kitaifa:

  • Vipigo: 22.3%
  • Ukatili wa kingono: 8.7%
  • Ndoa za utotoni: 32.4%
  • Maamuzi binafsi ya wanawake: 72%

Lakini katika mkoa wa Shinyanga, hali ni mbaya zaidi:

  • Vipigo: 34.2%
  • Ukatili wa kingono: 17.8%
  • Ndoa za utotoni: 45.9%
  • Maamuzi binafsi ya wanawake: 77%

Takwimu hizi zinaonesha kuwa Shinyanga inahitaji juhudi za makusudi kukabiliana na hali hiyo kupitia elimu endelevu, mabadiliko ya kifikra na ushirikiano wa karibu kati ya viongozi, wazazi na vijana.

Kaimu Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Hilda Ebunka, anaeleza kuwa hali ya mimba za utotoni imeanza kupungua kutokana na juhudi mbalimbali za utoaji wa elimu kwa jamii. Lakini bado anasisitiza kuwa jamii inapaswa kuendelea kushirikiana ili kulinda watoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni na vitendo vya unyanyasaji.

Afisa Ustawi wa Jamii, Paul Lupolaso, anabainisha kuwa ndoa za utotoni ni moja ya changamoto zinazokwamisha maendeleo ya watoto wa kike, huku akihimiza wazazi kuwapa watoto wao nafasi ya kufikia ndoto zao kwa kupitia elimu.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu, Inspekta Rose Mbwambo, anasisitiza kuwa jamii inapaswa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za ukatili mapema ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria. Anasema dawati hilo limekuwa kimbilio kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na limechangia kuwapa faraja na msaada wa kisheria wahanga wengi.

Wananchi kutoka kata za Idukilo, Mwamalasa, Ukenyenge na Mwamashele, wanaomba elimu iendelee kutolewa ambapo walisema wananchi wengi hawana uelewa jambo ambalo linasababisha matukio hayo ya ukatili kuendelea katika Wilaya ya Kishapu.

Shija Mongo wa kata ya Mwamashele anasema: “Tulikuwa tunaona haya kuzungumzia masuala ya ndoa za utotoni, lakini sasa tumeelewa kuwa ukimya wetu ni hatari kwa watoto wetu. Tumejifunza kuwa majadiliano ni silaha ya mabadiliko.”

Antony Francis kutoka Ukenyenge anaongeza: “Makundi rika ni njia nzuri ya kutengeneza sauti moja katika familia na jamii. Tunahitaji kuendelea kujifunza na kushirikiana kwa ajili ya kizazi bora.”

Ukatili wa kijinsia hauwezi kukomeshwa kwa sheria pekee. Unahitaji mabadiliko ya kifikra, ushirikiano wa jamii nzima, na nafasi ya mazungumzo ya wazi kati ya vijana na wazee kupitia midahalo ya makundi rika.

Post a Comment

Previous Post Next Post