Wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wamepewa taarifa ya ujio wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi watakaoanza kutoa huduma maalumu katika Hospitali ya Manispaa hiyo kuanzia tarehe 2 Juni hadi 6 Juni 2025.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Alexius Kagunze, ambapo amewakaribisha wananchi wote wa maeneo mbalimbali kufika na kupata huduma hizo muhimu za afya.
Huduma hizo zitapatikana kwa kutumia bima za afya (NHIF na ICHF) pamoja na malipo ya papo kwa papo (CASH), na zitatolewa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kila siku ndani ya siku hizo tano.
Mganga mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dkt. Elisha Robert amebainisha kuwa lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa wanawake wenye changamoto za kiafya zinazohusiana na afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake, na kwamba huduma hiyo ni fursa muhimu kwa wakazi wa Shinyanga kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa bila kusafiri kwenda mikoa mingine.
Post a Comment