" RAIS SAMIA: TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA JAMHURI YA MSUMBIJI

RAIS SAMIA: TANZANIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA JAMHURI YA MSUMBIJI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi wa Msumbiji katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri hiyo, ikiwa ni mwaliko maalum wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. Daniel Francisco Chapo. Sherehe hizi zimefanyika katika Uwanja wa Machava, Mjini Maputo, tarehe 25 Juni 2025.

Matukio mbalimbali wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri hiyo, ikiwa ni mwaliko maalum wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. Daniel Francisco Chapo. Sherehe hizi zimefanyika katika Uwanja wa Machava, Mjini Maputo, tarehe 25 Juni 2025.

……………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema

Tanzania itaendelea kushirikiana na Jamhuri ya Msumbiji katika kuleta maendeleo, ustawi

wa wananchi na kukuza mshikamano barani Afrika.

Akihutubia katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji

zilizofanyika leo katika Uwanja wa Machava, jijini Maputo, Rais Dkt. Samia amesema kuwa

uhusiano wa Tanzania na Msumbiji sio wa kijiografia pekee, bali una mizizi ya kihistoria

na mapambano ya pamoja dhidi ya ukoloni.

Rais Dkt. Samia amekumbushia historia ya mchango wa Tanzania katika harakati za

ukombozi wa Msumbiji kwa kuwapa hifadhi, licha ya kukabiliwa na changamoto za

kiuchumi na matishio ya kiusalama kutoka kwa waliokuwa wakoloni wa Msumbiji, na

amewatambua waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati

Samora Moisés Machel, kwa kuimarisha mshikamano wa kweli kati ya wananchi wa nchi

hizi mbili wakati wa harakati hizo.

“Tulikuwa tayari kuchelewesha maendeleo yetu ili kuhakikisha ndoto ya ukombozi wa

Msumbiji na mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika inatimia,” alisema Rais Dkt. Samia.

Vilevile, Rais Dkt. Samia amepongeza jitihada za Msumbiji, baada ya kupata uhuru wake,

katika kusaidia mataifa mengine ya Afrika kupata uhuru na kuishukuru Msumbiji kwa

msaada uliotoa kwa Tanzania wakati wa Vita ya Kagera dhidi ya uvamizi wa Nduli Idi

Amin, mwaka 1978–1979.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amepongeza hatua ya maendeleo iliyofikiwa na Jamhuri ya

Msumbiji katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo katika nyanja za elimu, afya na miundombinu, ambayo yaliletwa na dhamira ya kujenga jamii jumuishi na yenye
matumaini.
Katika hatua ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara, Rais Dkt. Samia ametangaza nia ya
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania
na Msumbiji mwishoni mwa mwaka huu.
Rais Dkt. Samia pia amewapongeza wananchi wa Msumbiji kwa kaulimbiu ya mwaka huu
ya Mbio za Mwenge wa Umoja wa Kitaifa: “Miaka 50: Kuwainua Wanawake, Kujenga
Usawa wa Kijinsia,” akisisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni msingi wa mapinduzi ya kweli
ya maendeleo.
Aidha, ametoa pongezi maalum kwa wanawake wapigania uhuru wa Msumbiji, akiwemo
Josina Muthemba Machel na wengine kwa ujasiri usio na kifani.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa mchango wa wanawake katika harakati za ukombozi wa
Msumbiji sio historia tu ya kupigiwa makofi, bali ni urithi wa kuenziwa na kizazi cha sasa
kwa kuwawekea wanawake mazingira wezeshi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo
ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Mapema leo, Rais Dkt. Samia alitembelea eneo la Kumbukumbu ya Mashujaa wa Nchi ya
Msumbiji (Heroes’ Square) jijini Maputo, ambako aliweka shada la maua kama ishara ya
heshima kwa mashujaa waliopoteza maisha yao wakipigania uhuru wa Msumbiji.
Rais Dkt. Samia atarejea nchini leo mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi Jamhuri
ya Msumbiji.
Shaaban Kissu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Post a Comment

Previous Post Next Post