" SALOME MAKAMBA ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UBUNGE WA VITI MAALUM CCM MKOA WA SHINYANGA

SALOME MAKAMBA ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UBUNGE WA VITI MAALUM CCM MKOA WA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Makamba, leo Juni 29, 2025, amechukua rasmi fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine, kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Makamba amekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Bi. Habiba Musimu, katika ofisi za chama hicho mkoani humo.

Akizungumza mara baada ya kupokea fomu, Salome amesema anaingia tena katika mchakato huo akiwa na nia thabiti ya kuendeleza mapambano ya maendeleo ya wanawake wa Mkoa wa Shinyanga kwa moyo wa uzalendo na kujitoa.

“Nina uzoefu, dhamira ya kweli na moyo wa kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake. Niko tayari kuendelea kuwatumikia kwa heshima kubwa,” amesema Makamba.

Mbunge huyo amesema kipindi chake cha awali kimemjengea uzoefu mkubwa katika kutetea haki na fursa za wanawake, na anaamini kuwa bado ana nafasi ya kuchangia zaidi maendeleo ya jamii hiyo, endapo atapewa ridhaa na chama.

Aidha Salome Makamba wakati anawasili ofisi hizo ameingia kwa kutumia baiskeli badala ya gari, akisema ni njia ya kuenzi na kudumisha asili ya maisha ya watu wa Shinyanga.

Ameeleza kuwa aliamua kutumia baiskeli kama njia ya kuonyesha mshikamano na wananchi wa kawaida, hasa wanawake na vijana wanaotegemea usafiri wa baiskeli katika shughuli zao za kila siku.

Uchukuaji wa fomu kwa nafasi mbalimbali ndani ya CCM unaendelea mkoani Shinyanga na maeneo mengine nchini, huku wagombea mbalimbali wakiendelea kujitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho tawala kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.Salome Makamba akiwasili kwa baiskeli katika ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Viti Maalum kupitia UWT.Salome Makamba akipokea fomu ya kugombea ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga kupitia UWT, katika ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

 

Post a Comment

Previous Post Next Post