" SHINYANGA: WAKAZI WALIOPOTEZA MAKAZI KWA MAFURIKO WASHUKURU COMPASSION TANZANIA KWA KUWAJENGEA NYUMBA MPYA ZA KISASA

SHINYANGA: WAKAZI WALIOPOTEZA MAKAZI KWA MAFURIKO WASHUKURU COMPASSION TANZANIA KWA KUWAJENGEA NYUMBA MPYA ZA KISASA

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga waliopoteza makazi yao kufuatia mafuriko ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali mwaka 2024, wameishukuru Compassion Tanzania kwa msaada wa kuwajengea nyumba mpya kupitia ushirikiano na makanisa saba ya kipentekoste na kiinjili yaliyoko katika manispaa hiyo.

Wakazi hao, ambao walikumbwa na athari za moja kwa moja za maafa hayo ya asili, wameeleza kuwa walijikuta wakikosa mahali pa kuishi, wakilala chini ya turubai huku wakikabiliwa na changamoto za chakula, usalama na afya.

Hali hiyo iliwaweka katika mazingira ya unyonge kwa kipindi kirefu hadi pale walipopata msaada kutoka kwa shirika hilo la kimataifa linalotoa huduma za maendeleo ya mtoto na familia maskini.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na viongozi wa Compassion Tanzania, jumla ya nyumba 29 zimejengwa katika kata saba za Manispaa ya Shinyanga, zikiwemo Kolandoto, Kitangili, Ndala, Masekelo na nyingine, kwa gharama ya shilingi 183,900,292.

Nyumba hizo zimejengwa kupitia vituo vya huduma kwa mtoto na kijana (Child and Youth Development Centers) vilivyo chini ya usimamizi wa makanisa saba ambayo ni EAGT Ndala, KKKT Mjini, Anglican Ndala, Anglikan Mjini, AICT Kitangili, AICT Kolandoto na TAG Moleka.

Mwenyekiti wa Compassion Tanzania, Lemi Dumbi, amesema mradi huo ni sehemu ya dhamira ya shirika hilo katika kuimarisha ustawi wa watoto na familia maskini nchini kwa kuwapatia si tu huduma za afya, elimu na lishe, bali pia mazingira salama ya kuishi.

“Tunatambua kuwa maendeleo ya mtoto hayawezi kufikiwa pasipo familia yake kuwa katika mazingira salama. Ndiyo maana tuliona ni muhimu kuingilia kati kwa vitendo baada ya maafa yale ya mwaka jana,” amesema Dumbi.

Naye mwenyekiti wa Klasta ya Shinyanga, Steven Simion, amesema kazi ya ujenzi wa nyumba hizo ilifanyika kwa hatua na usimamizi wa karibu wa makanisa yenye vituo vya watoto, huku jamii ikihusishwa katika utekelezaji ili kuhakikisha uendelevu.

Amesema shirika hilo limejikita katika kutoa huduma kwa watoto maskini wenye mazingira magumu na kwamba wanashirikiana na makanisa kama njia ya kuunganisha huduma za kiroho, kijamii na kimwili kwa mtoto na familia yake.

Katika hafla ya kukabidhi nyumba hizo kwa wanufaika, mgeni rasmi Said Kitinga, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, alilipongeza shirika la Compassion kwa kazi hiyo ya kijamii na kusema serikali itaendelea kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali yenye nia njema ya kusaidia jamii.

“Tunatambua mchango mkubwa wa mashirika ya kidini katika kusaidia serikali kutimiza wajibu wake kwa jamii. Tunapenda kuona zaidi mashirika kama Compassion yakisaidia wananchi wetu kwa vitendo kama hivi,” amesema Kitinya.

Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau wote wa maendeleo na kwamba juhudi za mashirika kama haya zinachangia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Wakati wa tukio hilo, Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga, Zakayo Bugota, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali na taifa kwa ujumla, hasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Tunaliombea taifa letu liendelee kuwa la amani na mshikamano. Tunatambua kuwa kazi hii ya kujenga nyumba ni sehemu ya huduma kwa jamii, lakini pia ni njia ya kuonyesha upendo wa Kristo kwa vitendo,” amesema Askofu Bugota.

Ameongeza kuwa makanisa yataendelea kushirikiana na serikali katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na huduma za kijamii, maadili na malezi bora ya watoto.

Baadhi ya familia zilizonufaika na nyumba hizo zimesema msaada huo umewarejeshea heshima na matumaini baada ya kipindi kirefu cha kuhangaika bila makazi maalum.

Wengine wamesema nyumba hizo zimewawezesha kurudi katika maisha ya kawaida, watoto wao sasa wanapata muda wa kusoma vizuri na familia zimerudishiwa heshima katika jamii.

Mradi wa ujenzi wa nyumba 29 kwa waathirika wa mafuriko katika Manispaa ya Shinyanga ni mfano hai wa ushirikiano kati ya mashirika ya kidini, jamii na serikali katika kusaidia watu walioko katika mazingira magumu.

Aidha, unatoa somo kuwa majanga ya asili yanapotokea, kunahitajika mshikamano wa kweli na hatua za haraka kuwanusuru wahanga badala ya kuachwa kwa muda mrefu bila msaada.

Kwa mujibu wa Compassion Tanzania, miradi kama hiyo itaendelea kutekelezwa kadri ya uhitaji na uwezo wa kifedha wa shirika hilo, huku vipaumbele vikiwa kwa watoto, familia na maeneo yenye changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii.

 


 

Post a Comment

Previous Post Next Post