Wakati bei ya mafuta ya petroli ikipanda kwa Sh29 mafuta ya dizeli imeshuka kwa Sh255 ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza bei mpya za mafuta zinazoanza kutumika leo Julai 9, 2025, imesema bei ya mafuta kwa petroli itauzwa Sh2,996 ikilinganishwa na Sh2,968 za bei ya Juni.
“Ongezeko hilo ni Sh29 sawa na asilimia 0.94 linalotokana na mafuta hayo kupanda katika soko la dunia na changamoto ya usafiri,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ambayo imethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa mamlaka hiyo Mbarak Hassan Haji.
Mbaraka amesema mafuta ya Dizel yatauzwa kwa Sh2,907 kwa mwezi huu kutoka Sh3,162 sawa na punguzo la Sh255 sawa na asilimia 8.06.
Kwa upande wa mafuta ya taa yamepungua kwa Sh150 ambapo kwa Julai lita moja itauzwa kwa Sh3,000 ikilinganishwa na Sh3,150 iliyouzwa Juni sawa na asilimia 4.76.
Mafuta ya ndege yamepungua Sh151, kutoka Sh2,521 ya Juni hadi Sh2,370 kwa lita moja itakayouzwa Julai mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 5.99.
Hata hivyo, Zura imesema sababu ya kupungua kwa bei za mafuta ya dizeli, taa na mafuta ya ndege kwa mwezi huu ni kutokana na kushuka bei ya ununuzi wa mafuta katika soko la dunia, kupungua gharama za uingizaji mafuta kutoka katika soko la dunia hadi Zanzibar na mabadiliko ya fedha za kigeni.
Zura hupanga bei hizo kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani.
Post a Comment