" MASHINE YA KUCHUNGUZA SARATANI YA MATITI KALOLENI MKOMBOZI WA JAMII

MASHINE YA KUCHUNGUZA SARATANI YA MATITI KALOLENI MKOMBOZI WA JAMII


Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.

Mashine ya kuchunguza Saratani ya Matiti iliyogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni mia nne imezinduliwa katika kituo cha afya cha Kaloleni Jijini Arusha, ambayo tayari imeanza kutoa huduma kwa wateja wake.

Akitoa taarifa  kuhusiana na mradi wa mshine hiyo Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dr. Anna Kimaro amesema mashine hiyo imekuwa mkombozi kwa wananwake na wanaume kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya matiti ambapo kati ya watu 569 waliopimwa kati yao 74 wamekutwa na maambukizi.

Ameongeza kuwa kati ya watu 100 waliopimwa mwanaume mmoja hukutwa na saratani na wengine 99 ni wanawake.

"Naishukuru Serikali kwa  kazi kubwa inayoendelea   kuifanya hususani sekta ya afya, wengi tuliowafanyia uchunguzi tumewakuta na hatua mbaya ya saratani, tumewapa rufaa kwenda hospitali kubwa, hii inatuonyesha kuwa tungekuwa tumepata mashine hii mapema wanawake hao wasingefikia hatua hiyo iwapo wangefanyiwa uchunguzi mapema",

"Hii ni nafasi ya pekee kwa mkoa wetu, kila mmoja mwenye umri zaidi ya miaka 35 kuchunguza afya ya matiti yake ili atibiwe mapema" amesema. Dr. Kimaro.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ismail Ali Ussi amewapongeza Madaktari wote nchini kwa kazi kubwa wanayoifanya kuwahudumia wagonjwa  usiku na mchana na kuhakikisha wanaokoa maisha yao.

"Kila mmoja ni shahidi kwamba serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza ahadi zake za kuleta maendeleo kwa wananchi, sasa ni zamu yenu wananchi kuchukua hatua za kuchunguza afya zenu na kuwatia moyo watumishi wa afya na sio kuwavunja moyo maana kazi yao sio rahisi"amesema Ussi.

Mwenge wa Uhuru umekamilisha shughuli zake za uzinduzi wa miradi, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi mkoani Arusha na unatarajiwa  kukabidhiwa Mkoani Manyara hapo kesho Julai 12, 2025.

_Watumishi wa Kituo cha Afya Kaloleni Jijini Arusha wakifurahia uzinduzi wa Mashine ya Saratani ya Matiti.

Post a Comment

Previous Post Next Post