Na RS SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameendelea na ziara zake za kikazi kwa kufanya kikao maalum na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, lengo kuu likiwa ni kujitambulisha rasmi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, pamoja na kueleza mwelekeo wa utendaji kazi anaoutarajia mkoani humo.
Amefanya ziara hiyo jana Julai 23,2025.
Katika hotuba yake mbele ya watumishi hao, Mhe. Mhita amewataka kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, na kushughulikia ipasavyo kero za wananchi.
Alisisitiza kuwa huduma bora kwa jamii ni msingi wa maendeleo ya kweli, hivyo kila mtumishi anatakiwa kuonyesha uzalendo, kujituma na kufanya kazi kwa kushirikiana.
Amesema kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele ni kuongeza mapato ya halmashauri kupitia vyanzo halali vya mapato bila kutumia nguvu kwa wananchi. Alieleza kuwa ukusanyaji wa mapato unapaswa kuzingatia weledi, ushirikishwaji na kutoa elimu kwa walipa kodi ili kufanikisha maendeleo ya halmashauri hiyo na mkoa kwa ujumla.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa rasilimali za umma, uwazi katika matumizi ya fedha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for money). Alionya dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka au upotevu wa fedha za umma.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Mhita aliwataka wakuu wa idara na vitengo kushirikiana kwa karibu na viongozi wa ngazi za chini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa wakati na kwa ufanisi.
Mara baada ya Mkuu wa Mkoa kumaliza hotuba yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Dkt alimpongeza kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo. Alimshukuru kwa kufika na kuzungumza na watumishi wa halmashauri, huku akiahidi kuwa ofisi yake itayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa.
Baada ya kikao hicho, Mhe. Mhita aliendelea na ziara kwa kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya halmashauri hiyo, ikiwemo miradi ya afya, elimu, na miundombinu. Alionesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, akiwataka wasimamizi kuhakikisha miradi inakamilika kwa viwango vya ubora unaotakiwa.
Katika kuhitimisha ziara yake, Mkuu wa Mkoa aliwaasa watumishi kuendelea kushikamana na kufanya kazi kwa bidii, akisisitiza kuwa maendeleo ya Mkoa wa Shinyanga yatafanikiwa kwa ushirikiano wa dhati kati ya serikali na wananchi.
Post a Comment