
Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Boniphace N. Butondo ameonyesha shukrani zake za dhati kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) huku akisisitiza mshikamano na mshirikiano ndani ya chama.
Kupitia ujumbe wake, Butondo amesema:
"Nimepokea uamuzi wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) kwa moyo wa unyenyekevu na shukrani, Maana Biblia inatufundisha kumshukuru Mungu kwa kila jambo. Hivyo sifa na utukufu ni kwa Mungu Pekee."
Aidha, Butondo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano aliyopata heshima ya kuwatumikia wananchi wa Kishapu kama Mbunge, amefanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa uaminifu na upendo mkubwa, hususan katika sekta za maji, afya, elimu, barabara na mawasiliano.
Amesema:
"Kwa miaka 5 niliyopewa heshima ya kuwatumikia wananchi wa Kishapu kama Mbunge, nimetekeleza majukumu yangu kwa uaminifu na upendo mkubwa ikiwa pamoja na kupambana maendeleo katika nyanja za Maji, Afya, Elimu, Barabara Na Mawasiliano na ni furaha yangu kuona mchango wangu umeacha alama za maendeleo katika jimbo letu."
Butondo pia amepokea kwa unyenyekevu uamuzi wa kamati kuu ya CCM Taifa wa kumteua Lucy Thomas Mayenga, akimpongeza na kumtakia kila la heri.
"Nimepokea kwa unyenyekevu uamuzi wa kamati kuu ya CCM Taifa kwa kumteua Ndugu Lucy Thomas Mayenga, nampongeza na kumtakia kila la heri. Uamuzi wa vikao vya chama chetu ni msingi wa umoja na mshikamano wetu, ni wajibu wetu kuuheshimu."
Akihitimisha, Butondo amewataka wanachama na wananchi kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi.
"Kwa pamoja tunalo jukumu moja la kuungana, kuondoa tofauti za makundi, na kushirikiana ili kuhakikisha Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mbunge wetu na Madiwani kata zote 29 za Kishapu tunapata ushindi wa kishindo. Mimi nipo tayari."
Post a Comment