" CHIFU ANTONIA SANGALALI AHIMIZA KUENDELEZA UTAMADUNI NA MILA ZA KISUKUMA

CHIFU ANTONIA SANGALALI AHIMIZA KUENDELEZA UTAMADUNI NA MILA ZA KISUKUMA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Machifu Tanzania ambaye pia ni Ntemi wa Himaya ya Jigoku (Masela) iliyopo Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Chifu Antonia Sangalali, ameendelea kusisitiza umuhimu wa jamii kuenzi na kuendeleza mila na desturi za asili ili kuhakikisha zinabaki kuwa urithi kwa vizazi vijavyo.

Chifu Sangalali ameyasema hayo Agosti 24, 2025 katika tamasha lake la utamaduni linalofanyika kila mwaka likiwa na lengo la kudumisha mshikamano wa kijamii kupitia urithi wa kabila la Wasukuma.

Amesema mila na desturi ni nguzo muhimu za maadili na mshikamano wa kijamii, hivyo ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha anawarithisha watoto wake ili kuendeleza misingi ya heshima na mshikamano wa jamii.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunawafundisha watoto wetu mila, desturi na historia ya asili zetu. Tukifanya hivyo tutakuwa tumelinda utambulisho wa jamii na taifa letu,” amesema Chifu Sangalali.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Anney, amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa viongozi wa kimila katika kulinda amani, mshikamano na maendeleo ya kijamii. Amesema serikali itaendelea kushirikiana na machifu katika kutunza historia na urithi wa utamaduni wa jamii hususan mkoa wa Simiyu.

Baadhi ya wananchi kutoka himaya ya Jigoku waliohudhuria tamasha hilo wamepongeza juhudi za Chifu Sangalali za kuhakikisha tamasha la utamaduni linaendelea kufanyika kila mwaka, wakibainisha kuwa limekuwa darasa muhimu la kujifunza historia na mila za Kisukuma, hasa kwa vijana.

Tamasha hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa kimila, wadau wa maendeleo na wananchi kutoka maeneo tofauti ya wilaya ya Maswa na mikoa jirani.

Aidha, burudani za ngoma za asili na nyimbo za kitamaduni zilipamba tamasha hilo ambapo wasanii maarufu wa muziki wa Kisukuma, Nhelemi Mbasando na Ng'wana Kang’wa, wametumbuiza na baadaye kukabidhiwa tuzo za heshima kama ishara ya kutambua mchango wao katika kuenzi na kuendeleza nyimbo za asili miongoni mwa jamii ya Wasukuma.

Mtemi Antonia Sangalali, akizungumza na wananchi wa himaya yake ya Jigoku (Masela) kwenye tamasha la utamaduni Agosti 24, 2025.

Mtemi Antonia Sangalali, akizungumza na wananchi wa himaya yake ya Jigoku (Masela) kwenye tamasha la utamaduni Agosti 24, 2025.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt. Vicent Anney akizungumza katika tamasha hilo la utamaduni himaya ya Jigoku 2025, ambapo amempongeza chifu Antonia Sangalali kwa kuendeleza utamaduni wa eneo hilo.






GUSA LINK HAPA CHINI👇


🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post