" MHANDISI JAMES JUMBE AMWAGA MILIONI 1.5 KUUNGA MKONO VIJANA WA KKKT EBENEZER KATIKA TAMASHA LA “TWENZETU KWA YESU”

MHANDISI JAMES JUMBE AMWAGA MILIONI 1.5 KUUNGA MKONO VIJANA WA KKKT EBENEZER KATIKA TAMASHA LA “TWENZETU KWA YESU”

Na Mwandishi wetu, Misalaba Media 

Mhandisi James Jumbe ameonesha tena moyo wa ukarimu na kujali maendeleo ya vijana kwa kumwaga shilingi milioni 1.5, fedha alizotumia kununua tiketi 300 kwa ajili ya kuwasapoti vijana na washiriki wa tamasha kubwa la “Twenzetu Kwa Yesu” linalosimamiwa na Kanisa la KKKT Ebenezer.

Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Jumamosi, Agosti 16, 2025, katika viwanja vya CCM Kambarage, likiwa na lengo la kuhamasisha mshikamano wa kijamii, kuimarisha imani na kuinua vipaji vya vijana wa Shinyanga.

Kwa kununua tiketi hizo na kuwapa bure kabisa, Jumbe ameonesha mfano wa kuigwa katika kuunga mkono shughuli za kijamii na kidini, hatua ambayo imepongezwa na waandaaji wa tamasha na wakazi wa Shinyanga.

Wakizungumza baada ya kupata taarifa za msaada huo, baadhi ya vijana wamesema msaada wa Jumbe si tu umewarahisishia ushiriki bali pia umeongeza hamasa ya kuhudhuria tamasha hilo kwa wingi.

Tamasha la “Twenzetu Kwa Yesu” mwaka huu linatarajiwa kuwa la kipekee, likijumuisha muziki wa injili, michezo, na mahubiri yenye mguso wa kiroho, huku vijana wakipewa nafasi ya kuonesha vipaji vyao mbalimbali.

Mhandisi Jumbe amekuwa akijulikana si tu kwa shughuli zake za kisiasa, bali pia kwa kujitolea mara kwa mara katika masuala ya kijamii na maendeleo ya vijana ndani na nje ya Shinyanga.


Post a Comment

Previous Post Next Post