
Kijana na mwanasiasa mzoefu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Kizumbi, Peter Alex Frank maarufu kama Mr. Black, ameonyesha hekima na uungwana wa kisiasa baada ya kutangaza msimamo wake kufuatia matokeo ya kura za maoni za wagombea udiwani.
Katika kinyang’anyiro hicho kilichovuta hisia za wanachama wengi, Mr. Black alimaliza nafasi ya pili kwa kupata kura 151, huku aliyeshika nafasi ya kwanza akipata kura 174. Pamoja na tofauti hiyo ndogo, Mr. Black amesema anakubali kwa moyo wa dhati maamuzi ya chama na ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha CCM inapata ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza mara baada ya matokeo, Mr. Black amewahimiza wale wote waliotia nia lakini hawakuteuliwa kuwa na subira na mshikamano kwa maslahi mapana ya chama. Ametoa wito wa kuvunja makundi na kusimama kama familia moja, akisisitiza kuwa mshindi wa kweli ni CCM na si mtu mmoja mmoja.
Aidha, amewashukuru wananchi wa Kata ya Kizumbi kwa upendo na imani waliomwonyesha wakati wa kura za maoni, akiahidi kuendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika kuliletea maendeleo eneo hilo.
“Ni wakati wa kuombea uchaguzi wa amani na mshikamano, ushindi wa kishindo wa CCM upatikane Shinyanga mjini kwa jimbo lote na kata zote,” amesema Mr. Black huku akiahidi kuendelea kutoa hamasa na mshikamanio wa chama chake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Post a Comment