
Na Mapuli Kitina Misalaba
Shirika la Youth and Women Emanapation (YAWE) kwa kushirikiana na shirika la Restless Development limefanya kikao cha mwezi chenye lengo la kutoa elimu na mapendekezo kuhusu kodi ya majengo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika ulipaji kodi.
Kikao hicho kimefanyika kupitia mradi uitwao “Kijana Wajibika: Ijue Kodi Yako, Shiriki na Lipa” unaofadhiliwa na IBP, ukiwa na dhamira ya kuwajengea vijana uelewa juu ya wajibu wao katika kukuza mapato ya Serikali kupitia kodi.
Katika kikao hicho, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Victor Kajuna ameeleza aina mbalimbali za kodi zinazohusika katika ngazi ya wananchi na wafanyabiashara, pamoja na kutoa mwongozo wa upatikanaji wa leseni. Elimu hiyo inalenga kuwawezesha vijana kuepuka changamoto za kisheria na kibiashara pindi wanapoendesha shughuli zao.
Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo, Bi. Dotto Kahabi, amewakumbusha vijana kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri. Amefafanua masharti ya kupata mikopo hiyo, ikiwemo uundwaji wa vikundi rasmi, usajili wa vikoba, na taratibu za benki.
Bi. Kahabi amesisitiza kuwa mikopo hiyo ni nyenzo muhimu ya kuwainua vijana kiuchumi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, sambamba na ulipaji kodi unaosaidia kuboresha huduma za kijamii.
Washiriki wa kikao hicho wamepewa nafasi ya kufanya mijadala na kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu kodi ya majengo, hatua iliyolenga kuhakikisha sauti za wananchi, hususan vijana, zinazingatiwa katika sera na maamuzi ya Serikali.
Baadhi ya vijana walioshiriki wamepongeza na kushukuru kwa elimu waliyoipata, huku wakiahidi kuwa mabalozi wa ulipaji kodi na kuwahamasisha wenzao kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Peter Joseph kutoka shirika la YAWE amesema elimu hiyo itakuwa endelevu na itaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga, ili kuongeza ushiriki wa vijana katika ujenzi wa taifa.
Amesema lengo kubwa ni kuona vijana wanatambua nafasi yao, wanashiriki kikamilifu kwenye kulipa kodi, na pia kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.
Afisa Biashara wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Victor Kajuna akitoa elimu.




Post a Comment