Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka wakati akiwasilisha mada maalum kuhusu Utangazaji wa Migogoro na Maafa Kipindi cha Uchaguzi kwenye mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 uliofanyika Agosti 3,2025 Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Na Kadama Malunde – Malunde1 Blog
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wazalishaji wa maudhui mtandaoni pamoja na vyombo vya habari kwa ujumla kuzingatia weledi, maadili ya taaluma ya habari na wajibu wao kwa jamii hasa katika kipindi nyeti cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza Jumapili, Agosti 3, 2025 katika Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni uliofanyika Mlimani City, Dar es Salaam, Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, amewasilisha mada kuhusu “Utangazaji wa Migogoro na Maafa Kipindi cha Uchaguzi”, akiainisha nafasi muhimu ya vyombo vya habari katika kulinda amani, mshikamano wa kitaifa na haki za wananchi.
Mhandisi Kisaka amebainisha kuwa, vipindi vya uchaguzi mara nyingi huambatana na ongezeko la mijadala kinzani na ni katika kipindi hicho upotoshaji wa taarifa mitandaoni huongezeka, hivyo kuna haja kwa vyombo vya habari na wazalishaji wa maudhui kuhakikisha wanakuwa chachu ya uwazi, uelewa na mshikamano wa kitaifa kwa kuchagua taarifa zinazojenga na kuelimisha.
“Vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee ya kuimarisha utulivu kwa kuwasilisha taarifa kwa uwiano, kuchochea mijadala ya staha na kutoa majukwaa kwa wagombea na wananchi kubadilishana mawazo kwa njia ya heshima,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa, wajibu wa wanahabari na wazalishaji wa maudhui ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazolinda usalama wa jamii, kuimarisha amani katika mchakato wa uchaguzi, kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wapiga kura na wananchi wote.
Amekumbusha pia umuhimu wa kuepuka lugha ya matusi, kejeli au uchochezi, hasa katika kuripoti matukio yanayohusisha siasa. Alieleza kuwa lugha ni silaha yenye uwezo wa kuchochea au kuleta utulivu, hivyo waandishi wanapaswa kuwa makini katika kuchagua maneno yao.
“Wakati mwingine si lazima kuripoti kila kauli ya kuchochea, bali tumieni weledi kuhakikisha mnazipa nafasi kauli zinazojenga na kulaani vurugu. Hii ni sehemu ya majukumu yenu katika kujenga jamii yenye mshikamano,” ameongeza Mhandisi Kisaka.
Katika muktadha wa kuripoti uchaguzi wakati wa maafa, amesisitiza umuhimu wa kuripoti kwa uwiano, usahihi na bila upendeleo huku wakizingatia muktadha wa kijamii, kiuchumi na kisiasa, hususan jinsi majanga yanavyoweza kuathiri utekelezaji wa haki ya kupiga kura kwa makundi maalumu kama watu wenye ulemavu, wazee na wahanga wa maafa.
Amehimiza pia kuzingatia utu wa mpiga kura kwa kutumia takwimu sahihi, kuepusha upotoshaji na kusaidia jamii kuwa na uelewa sahihi wa mchakato mzima wa uchaguzi.
Mkutano huo uliobeba kaulimbiu “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura” ulihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari kwa lengo la kujengeana uelewa na uwezo wa kutoa taarifa kwa weledi wakati wa uchaguzi.
Post a Comment