" VIJANA 157 WA COMPASSION INTERNATIONAL CLUSTER ZA SHINYANGA NA KAHAMA WAHITIMU, WAASWA KUTUMIA UJUZI KWA MAENDELEO YA JAMII NA TAIFA

VIJANA 157 WA COMPASSION INTERNATIONAL CLUSTER ZA SHINYANGA NA KAHAMA WAHITIMU, WAASWA KUTUMIA UJUZI KWA MAENDELEO YA JAMII NA TAIFA

 

Na Elisha Petro, Misalaba Media

Vijana 157 kutoka katika vituo 14 vya Shirika la Compassion International Tanzania Cluster ya Shinyanga na Kahama, wamehitimu baada ya miaka 22 ya utumishi wao, huku wakihimizwa kutunza na kutumia vyema ujuzi na maarifa waliyoyapata ili kujikwamua kiuchumi na kuwa msaada kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo  Mhe. Pelesi Kamgisha, wakati wa mahafali ya kwanza ya vituo vya maendeleo ya mtoto na kijana cluster ya Shinyanga na Kahama yaliyofanyika katika kanisa la KKKT Ebeneza  Dayosisi ya Shinyanga lililopo Manispaa ya Shinyanga.

“Kwa sasa kundi kubwa katika jamii, hususan vijana, wapo katika janga la ukosefu wa ajira. Nawashauri kutumia vyema ujuzi na maarifa mliyoyapata ili muweze kuajiriwa au kujiajiri bila kuchagua kazi, kwani fursa zilizopo katika jamii zipo ndani ya taaluma mliyoipata.” - Amesema Mhe. Kamgisha 

Kwa upande wake, muwezeshaji wa Shirika la Compassion International Tanzania cluster ya Shinyanga na Kahama  Bw. Remmy Dumbi, ameyapongeza makanisa yote yenye vituo vya cluster kwa ushirikiano wanaoendelea kuuonyesha kwa watoto na vijana kwa kuwa unawasaidia kufikia ndoto na malengo yao.

 “Ushirikiano huu mnaouonyesha ni mzuri na muhimu zaidi kwa vijana wetu kwa sababu unawasaidia pakubwa   kufikia ndoto na malengo yao.”

Aidha, Mwenyekiti wa watendakazi Cluster ya Kahama ambaye pia ni mratibu wa kituo cha FPCT Shalom TZ 823 Bi. Renea Enos amesema wanajivunia mafanikio wanayoyapata vijana hao kwani yanaendelea kuwa chachu kwa vijana wengine waliokata tamaa na maisha.

"Tunamshukuru Mungu kwa mafanikio wanayoyapata vijana wetu na kikubwa tunajivunia kwa hawa vijana wanaohitimi leo kwa sababu wengi wao wamejiajili wapo waliokuja wakiwa wadogo lakini tumewalea katika misingi na wamekuwa chachu kwa vijana wengine waliopotea na kukata tamaa, Mkoa wetu huu mwitikio wa Elimu ulikuwa chini sana lakini ujio wa Compassion umeleta chachu sana na Elimu imekuwa na mwamko mkubwa sana"

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Zakayo Bugota, aliwasihi vijana hao kushiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025 kwa kutokuwa chanzo cha machafuko nchini.

Baadhi ya  wahitimu wamelishukuru shirika la Compassion Tanzania kwa kuwezesha uwepo wa vituo vya cluster katika makanisa mbalimbali, ambavyo vimewajengea uwezo wa kifikra na kuwapatia stadi mbalimbali za maisha zinazowaandaa kuajiriwa na hata kujiajiri.

 “Tunalishukuru Shirika la Compassion Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuanzisha vituo vya cluster katika makanisa mbalimbali, ambavyo vinatujenga na kutuandaa vyema kuishi maisha ndani ya jamii zetu. Leo kumekuwepo na uhaba wa ajira; vijana wengi wanahangaika kutafuta kazi, wengine wanapata, wengine wanakosa na kukata tamaa. Lakini shirika hili limekuwa msaada mkubwa kwetu kwa kutupatia ujuzi na maarifa mengi yanayotuwezesha kuingia katika soko la ajira na hata kujiajiri sisi wenyewe.”

Mahafali hayo yamehudhuriwa na wachungaji wa makanisa mbalimbali,viongozi wa serikali, wazazi wa wanafunzi wahitimu na wawakilisha wa taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo cha Afya Kolandoto, Chuo cha ufundi stadi (VETA) Shinyanga , Chuo cha St. Francis na chuo kikuu cha ushirika tawi la  Shinyanga. 

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo  Mhe. Pelesi Kamgisha, akizungumza.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo  Mhe. Pelesi Kamgisha, akizungumza.
Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Zakayo Bugota, akizungumza.
Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Zakayo Bugota, akizungumza.











Post a Comment

Previous Post Next Post