![]() |
Miongoni mwa waliokuwa wakigombea nafasi ya kuteuliwa kuwania nafasi ya Ubunge jimbo la Chemba wakiwa katika picha ya pamoja |
Na Seif Mangwangi, Chemba
Baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Chemba wameibua malalamiko kuhusu mchakato wa uchaguzi wa ndani kuchagua mgombea wa nafasi ya ubunge uliofanyika hivi karibuni, wakidai kuwa taratibu muhimu za chama hazikuzingatiwa.
Kwa mujibu wa barua ya malalamiko iliyowasilishwa kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma pamoja na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, wanachama hao wamesema katika uchaguzi huo baadhi ya wanachama walipiga kura bila ya kuwa na kadi za uanachama za CCM kinyume na taratibu pamoja na mwongozo wa CCM.
Kanuni za uchaguzi ndaza Chama cha Mapinduzi (CCM), zinataka wajumbe halali wanaoruhusiwa kupiga kura wagombea wanaowania nafasi ya ubunge au udiwani ndani ya chama kuwa na kadi za uanachama na sio kutumia kadi ya mpiga kura au kitambulisho cha wa Taifa (NIDA),
“Kupiga kura kwa kutumia kadi ya mpiga kura ni wapiga kura wa vyama vyote, kanuni zinataka Uchaguzi wa ndani lazima upigwe na wanachama wa chama husika kwa kutumia kadi zao za uanachama, hapa chemba hali ilikuwa tofauti, watu wamekuja na vitambulisho vya NIDA na wengine vya INEC wakaruhusiwa kupiga kura, sisi hili hatulikubali,” ilisema barua hiyo kwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM.
Aidha, katika madai yao wanachama hao wamepinga matokeo yaliyompa ushindi wa kishindo Kunti Majala, ambaye alihamia CCM kutoka chama pinzani, wakisema hali hiyo inazua maswali kuhusu uhalali wa mchakato mzima.
“Umeona wapi mtu ametoka Chadema halafu akakubalika jimboni kwa wana CCM kwa asilimia mia moja? huo ni mtihani umevuja majibu, na mtihani huo unatakiwa kufutwa,” walisema.
Katika uchaguzi huo wa wilaya ya Chemba, kulikuwa na wagombea sita ambapo Kunti Majala aliibuka mshindi kwa kura 5,809, akifuatiwa na Juma Nkamia aliyepata kura 1,220.
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Amina Bakari aliyepata kura 784, akifuatiwa na Omar Futo kura 408, Khamis Mkotya kura 196, na Fransis Julius kura 109.
Wanachama hao wamesisitiza kuwa chama kinapaswa kuzingatia maoni ya wananchi wa maeneo husika, kwani wao ndio wanaomfahamu vema kiongozi wanayemtaka.
“Tumeandika barua kwa viongozi, tunataka kujua kama zimefanyiwa kazi, ushauri wetu ni chama kiwasikilize wananchi wa chemba nani wanamtaka. Uchaguzi wa ndani ukiharibika, chama kitabeba mzigo mkubwa kwenye uchaguzi mkuu utakaojumuisha wagombea wote,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu na Michuzi Blog, Katibu wa CCM Wilaya ya Chemba, Moza Abdallah, alikiri kuwa baadhi ya wanachama walitumia kadi za NIDA au kadi za mpiga kura badala ya kadi za uanachama wa CCM.
Alithibitisha pia kuwa baadhi ya wagombea walikataa kusaini matokeo yaliyompa ushindi Kunti Majala.
“Ni kweli kulikuwa na changamoto, wapo wanachama walitumia kadi zisizo za chama na baadhi ya wagombea hawakusaini matokeo, hata hivyo, taarifa hizi tumeshazifikisha ngazi za juu kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Abdallah.
Wanachama hao wametoa wito kwa viongozi wa juu wa chama kuingilia kati sakata hilo na kuhakikisha uchaguzi wa ndani unakuwa wa haki, wakisisitiza kuwa uchafuzi siyo uchaguzi
Post a Comment