Na Mapuli Kitina Misalaba
Serikali inaendelea na jitihada za kuwaokoa wachimbaji 25 waliokuwa wamefunikwa na udongo katika machimbo ya Nyandolwa wilayani Shinyanga, ambapo hadi sasa watu watano wameokolewa.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amesema leo Agosti 16, 2025 kuwa kati ya watano hao, wawili wamefariki dunia na watatu wako hai.
Amefafanua kuwa wawili tayari wamekabidhiwa kwa ndugu zao na mmoja amepewa rufaa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Mtatiro amesema juhudi za uokoaji zinaendelea, na tayari wataalamu wamewabaini wachimbaji wawili wakiwa ndani ya udongo huku kazi ya kuondoa vikwazo ili kuwafikia ikiendelea.
Kwa upande wao, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo, na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stephine Kiruswa, wametoa pole kwa wananchi na kuwataka waendelee kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea na jitihada za uokoaji.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 katika Mgodi wa Wachapa Kazi, Nyandolwa, ambapo watu 25 walifukiwa wakiwa kwenye shughuli za ukarabati wa maduara.
Post a Comment