" ZAIDI YA WANANCHI 500 SHINYANGA WAPATA HUDUMA ZA KIBINGWA ZA MOYO KUPITIA KAMBI YA MADAKTARI WA JKCI

ZAIDI YA WANANCHI 500 SHINYANGA WAPATA HUDUMA ZA KIBINGWA ZA MOYO KUPITIA KAMBI YA MADAKTARI WA JKCI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Zaidi ya wananchi 500 wa Mkoa wa Shinyanga wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo kupitia Kambi Maalumu ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kuanzia Agosti 18 na kuhitimishwa leo Agosti 22, 2025.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Luzila John, amesema lengo la kambi hiyo lilikuwa ni kusogeza huduma za matibabu ya moyo karibu na wananchi na wakati huohuo kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika ngazi ya hospitali ya rufaa pamoja na hospitali za halmashauri.

Ameeleza kuwa kwa siku moja walitarajia kuhudumia wastani wa wananchi 100, lakini idadi iliongezeka ambapo kwa siku tano zaidi ya wananchi 500 walihudumiwa.

Aidha, jumla ya wataalamu wa afya 15 kutoka Hospitali ya Rufaa na hospitali za wilaya wamenufaika kwa mafunzo ya vitendo kutoka kwa madaktari hao bingwa.

Dk. Luzila ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha huduma za kibingwa zinasogezwa karibu na wananchi, hatua aliyosema imekuwa faraja kubwa kwa wakazi wa mikoa ya pembezoni.

Amesema pamoja na kambi hiyo kumalizika, wananchi waendelee kujitokeza kwenye kliniki za magonjwa ya moyo zinazotolewa hospitalini hapo kila Jumanne na Ijumaa.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa moyo kutoka JKCI, Dkt. Mlagwa Yango,  amesema wakati wa kambi hiyo wamebaini changamoto nyingi ikiwemo shinikizo la juu la damu na moyo kushindwa kufanya kazi vizuri.

Amesema wagonjwa 50 kati ya waliopimwa wamepelekwa rufaa kwenda kupata matibabu zaidi katika taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

Nao baadhi ya wananchi waliopata huduma wameishukuru serikali kwa kuwaletea madaktari bingwa hao na wameomba kambi hiyo iwe inafanyika mara kwa mara ili kusaidia jamii kupata huduma karibu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Luzila John, akizungumza na waandishi wa habari.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Luzila John, akizungumza.

Daktari bingwa wa moyo kutoka JKCI, Dkt. Mlagwa Yango, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 22, 2025.

Post a Comment

Previous Post Next Post