" MADEREVA WA PIKIPIKI SHINYANGA WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MAKUTANO YA MZUNGUKO BARABARANI

MADEREVA WA PIKIPIKI SHINYANGA WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MAKUTANO YA MZUNGUKO BARABARANI

Madereva wa pikipiki wanaojishughulisha na usafirishaji wa abiria (bodaboda) katika Manispaa ya Shinyanga wamepewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya makutano ya mzunguko barabarani (roundabout) ili kupunguza na kuzuia ajali zinazojitokeza mara kwa mara katika maeneo hayo.

Elimu hiyo imetolewa na Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Sajenti David Ndimila, ambapo ameeleza kuwa makutano ya mzunguko ni maeneo yanayohitaji umakini mkubwa kwa madereva wote, akisisitiza kwamba ajali nyingi hutokea kutokana na madereva kutokuwa na uelewa wa taratibu za matumizi ya barabara hizo.

“Madereva wengi hawafahamu utaratibu sahihi wa nani anayepaswa kupita kwanza katika roundabout, jambo linalosababisha vurugu na ajali zisizo za lazima. Ni muhimu kumpa kipaumbele dereva aliye ndani ya mzunguko na kuepuka mwendokasi unapokaribia eneo hili,” alisema Sajenti Ndimila.

Aidha, amewakumbusha madereva kuacha tabia ya kupita vyombo vingine vya moto mara tu wanapoingia kwenye mzunguko, kwani hatua hiyo inaweza kusababisha ajali kubwa.

Sajenti Ndimila pia amewahimiza madereva hao kuwa mabalozi wa usalama barabarani kwa kuwafundisha wenzao ambao hawakuhudhuria mafunzo hayo.

“Uelewa wenu utasaidia kupunguza ajali na kuokoa maisha. Hivyo ni wajibu wenu kushirikisha wengine elimu hii ili kila dereva aendeshe kwa uangalifu na kufuata sheria,” alisisitiza.

Kwa upande wao, baadhi ya madereva wa bodaboda waliokuwepo katika mafunzo hayo walishukuru kwa elimu waliyoipata, wakisema kuwa itawasaidia kuboresha uendeshaji wao na kuepuka migongano na askari wa usalama barabarani.

Elimu hii ni sehemu ya jitihada za serikali na vyombo vya usalama barabarani kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, sambamba na kupunguza ajali zinazotokana na uzembe na kutokujua sheria za usalama barabarani.

 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post