" MJASIRIAMALI WA UUZAJI WA KEKI ATOA USHAURI KATIKA MAONESHO YA KEKI MWANZA

MJASIRIAMALI WA UUZAJI WA KEKI ATOA USHAURI KATIKA MAONESHO YA KEKI MWANZA

Na Mwandishi wetu, Misalaba Media

Mjasiriamali anayejiusisha na uuzaji wa keki katika maeneo ya Ghandi Hall, Jijini Mwanza, Flora Charles kutoka Mkoa wa Simiyu, amepongeza maonesho ya keki na upishi wake akisema ni fursa kubwa kwa vijana na wajasiriamali kujifunza mbinu bora za kutengeneza na kuuza bidhaa hizo.

Akizungumza katika maonesho hayo, Flora alisema kuwa amefurahi kushiriki tukio hilo kwani limempa uelewa wa kina kuhusu namna ya kuboresha bidhaa zake ili kukidhi mahitaji ya wateja wa rika na ladha tofauti.

“Maonesho haya yameniwezesha kupata mbinu mpya za utengenezaji na uuzaji wa keki. Nimejifunza pia umuhimu wa kutumia viambato vyenye afya ili kuwavutia wateja na kuhakikisha bidhaa ninazouza zinakuwa salama kwa matumizi ya kila mtu,” alisema Flora.

Flora aliongeza kuwa kupitia maonesho hayo amepata nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya upishi na vifaa vya kutengeneza keki, jambo litakalomsaidia kupanua biashara yake na kuongeza ajira kwa vijana katika mkoa wake.

Aidha, aliwataka vijana na wanawake kutumia fursa kama hizi kujifunza ujuzi mpya badala ya kukaa bila shughuli, akisisitiza kuwa soko la keki linaendelea kukua kutokana na ongezeko la matukio ya sherehe na kijamii.

“Biashara ya keki ina nafasi kubwa ya kukuza kipato na kupunguza changamoto ya ajira. Tunachohitaji ni kujifunza na kuwekeza katika ubunifu na ubora,” aliongeza.

Maonesho hayo yameendelea kuvutia wananchi kutoka maeneo mbalimbali huku yakitoa nafasi kwa wajasiriamali kama Flora kuonesha bidhaa zao na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa sekta ya upishi.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

 

Post a Comment

Previous Post Next Post