Na.Osama Mohamedi -Songea Chuo cha VETA Songea kimefanya mahafali kwa wanafunzi 184 waliomaliza mafunzo ya mwezi mmoja kupitia Programu Maalum ya Wanawake na Samia, iliyolenga kuwapa wanawake ujuzi katika fani mbalimbali zikiwemo mapambo, kompyuta na ushonaji.Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia stadi zitakazowasaidia kuanzisha shughuli zao binafsi za kiuchumi.Akizungumza wakati wa kufunga rasmi mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Mtela Mwampamba, aliwataka wahitimu hao kutumia ujuzi walioupata kwa kujiunga kwenye vikundi vya kiuchumi ambavyo vitawawezesha kupata mikopo kupitia halmashauri na taasisi nyingine za fedha.> “Ni muhimu kuunda vikundi imara vitakavyowawezesha kupata mikopo kama mtaji wa kuanzia. Lakini muwe makini, si kila kikundi kinaweza kukopesheka – kuna vikundi ambavyo vina sifa hafifu na haviaminiki,” alisema Mwampamba.Aidha, aliwataka wahitimu hao kuwa wabunifu na kutumia fursa zinazopatikana katika mazingira yao kwa ajili ya kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kujifunza hata baada ya mafunzo rasmi.Programu Maalum ya Wanawake na Samia ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi yenye tija.Baadhi ya wahitimu walieleza kufurahishwa kwao na mafunzo hayo, wakisema yamewafungua macho na kuwapa matumaini mapya ya kujitegemea.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment