Na Mapuli Kitina Misalaba
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)
katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, Paschal Patrobas Katambi, amewaomba wananchi wa
Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano mkubwa wa kampeni
utakaohusisha ujio wa Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais wa CCM, Dkt. Emmanuel
Nchimbi, ambaye anatarajiwa kuwasili mkoani Shinyanga kesho Septemba 3, 2025.
Katambi ameyasema hayo leo Septemba 2, 2025 alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari, akibainisha kuwa mkutano huo utakuwa fursa
muhimu kwa wananchi kusikiliza kwa kina sera, mafanikio na Ilani ya CCM
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema wananchi wa Shinyanga wanapaswa kujitokeza kwa
wingi siyo tu kumsikiliza Dkt. Nchimbi, bali pia kupata elimu ya moja kwa moja
kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka
mitano iliyopita, pamoja na mipango mipya ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo
kupitia Ilani ya CCM 2025–2030.
“Wananchi wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi kwenye
ujio wa Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, wasikilize
sera za CCM kupitia Ilani yetu na kufahamu pia kuhusu Shinyanga Mpya ya
2025–2030,” amesema Katambi.
Katambi ameongeza kuwa katika mkutano huo viongozi wa
chama na wagombea watatoa maelezo ya kina kuhusu hatua kubwa za kimaendeleo
zilizofikiwa katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo elimu,
afya, barabara, maji na ajira, ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuinua
maisha ya wananchi wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, amesisitiza kuwa ujio wa Dkt. Nchimbi ni ishara
ya kujali mkoa wa Shinyanga na ni nafasi kwa wananchi kuonyesha mshikamano wao
na chama kwa kujitokeza kwa wingi ili kusikiliza, kuuliza maswali na kushiriki
katika mjadala wa maendeleo ya taifa kupitia Ilani ya CCM.
Kesho Septemba 3, 2025, Dkt. Emmanuel Nchimbi anatarajiwa kuwasili rasmi mkoani Shinyanga kwa ajili ya kampeni hizo za kunadi sera na ilani ya chama hicho, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment