Na Mwandishi wetu
Bukoba
Katika kutekeleza miradi ya maendeleo, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kupitia timu ya uratibu wa kuhamisha makaburi ya Kishenge imekutana leo na wananchi wanaodhaniwa kuwa ndugu wa marehemu waliolazwa kwenye makaburi hayo, kwa ajili ya majadiliano.
Kikao hicho kililenga kuwafahamisha wananchi hao kuhusu mpango wa Serikali, kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa, wa kutwaa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa soko kubwa litakaloweza kuhudumia wafanyabiashara zaidi ya 2,000.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Ndugu Jacob Nkwera, alisema:
"Tulipata nafasi ya kuandaa maandiko ya kuomba fedha za miradi, na sasa tumeidhinishiwa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa complex kubwa.
"Mji wetu ni mdogo na maeneo mengi yamebana, ndio maana tukaamua kuomba kutumia eneo hili la Kishenge.” alisema Nkwera.
Aidha, ameongeza kuwa pamoja na matangazo yaliyotolewa kupitia mitaani na vyombo vya habari, lisingekuwa jambo la busara kuanza mchakato bila kuzungumza na wananchi ambao ni wahusika muhimu.
Kwa kauli moja, wananchi walioridhia mchakato huo waliitaka Halmashauri kuendelea nao huku wakisisitiza umuhimu wa kushirikishwa katika kila hatua ya utekelezaji.
Ikumbukwe kuwa, Halmashauri tayari imeandika na kutuma nyaraka kwenye ofisi ya Waziri wa Ardhi na Februari 11, mwaka huu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratias Ndejembi (MB), alitembelea eneo hilo kujionea hali kabla ya kutoa kibali cha kuhamisha makaburi yanatarajiwa kuhamishiwa kwenye kiwanja kilichopimwa, kilichopo kata ya Buhembe.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment