Abiria wanaosafiri masafa marefu wametakiwa kujitambua na kuchukua tahadhari kwa kuepuka kushushwa katika maeneo yasiyo rasmi na yenye hatari, ili kujikinga na ajali zisizo za lazima.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Shinyanga, ASP Zainabu Mangara, wakati akitoa elimu kwa abiria kuhusu usalama barabarani na umuhimu wa kufuata taratibu sahihi za kushuka kwenye magari ya abiria.
ASP Mangara amesema baadhi ya abiria wamekuwa wakikubali kushushwa njiani, hata katika maeneo yenye mteremko, kona au vivuko vya watembea kwa miguu, jambo ambalo linaongeza uwezekano wa kutokea kwa ajali.
“Ni muhimu kuhakikisha mnakamilisha safari zenu kwa kushuka katika vituo rasmi vilivyotengwa. Mkishirikiana katika hili, mtakuwa mmechangia kwa kiasi kikubwa kulinda maisha yenu na ya wengine,” amesema ASP Mangara.
Aidha, amewataka madereva wa magari ya abiria kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na maadili ya kazi zao, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha abiria wanashushwa katika maeneo salama pekee.
ASP Mangara ameongeza kuwa madereva wanapaswa kujisimamia kwa uadilifu kwa kuwa wamepata mafunzo ya udereva na wanatambua vizuri sheria za usalama barabarani, hivyo hawapaswi kushusha abiria katika maeneo hatarishi kwa visingizio vyovyote.



Post a Comment