Na Moshi Ndugulile.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) mkoani humo, katika juhudi za kudumisha na kulinda amani ya Taifa.
Akizungumza na viongozi wa jumuiya hiyo ofisini kwake leo, Rc Mhita amesema viongozi wa JMAT wana jukumu kubwa la kuendeleza maadili ya umoja wa kitaifa, na kutumia nafasi zao kuhubiri upendo, mshikamano na maridhiano miongoni mwa wananchi.
“Ni muhimu viongozi wa dini na makundi ya kijamii kuwa makini na watu au makundi yenye ajenda za kugawa taifa kwa misingi ya dini au kabila,kwa maslahi yao binafsi. Badala yake, tuimarishe umoja na maridhiano kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa na Taifa,” amesema Mhita.
Ameongeza kuwa nafasi ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani ni muhimu katika kusaidia serikali kudumisha utulivu, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kutatua changamoto zake kwa njia ya mazungumzo yenye maridhiano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, ameahidi kuwa jumuiya hiyo itaendeleza jitihada za kuhakikisha amani, umoja na mshikamano vinadumu miongoni mwa wakazi wa mkoa huo.
Jumuiya hiyo inaundwa na viongozi wa dini, wazee wa mila, pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii.
Ni mara ya kwanza kwa viongozi wake kukutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, tangu Mhe. Mboni Mhita alipoteuliwa kuongoza Mkoa wa Shinyanga.
Mwisho










Post a Comment