" VIONGOZI WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM WAZUNGUMZA NA WAFANYABIASHARA WA SOKO LA KAMBARAGE SHINYANGA, WAHAMASISHA USHIRIKI WA KUPIGA KURA KUWACHAGUA WAGOMBEA WA CCM.

VIONGOZI WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM WAZUNGUMZA NA WAFANYABIASHARA WA SOKO LA KAMBARAGE SHINYANGA, WAHAMASISHA USHIRIKI WA KUPIGA KURA KUWACHAGUA WAGOMBEA WA CCM.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, viongozi wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka ngazi ya taifa na wilaya ya Shinyanga Mjini wameendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura, huku wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja na uzalendo.

Ziara hiyo imefanyika leo Oktoba 6, 2025 katika soko la Kambarage Mjini Shinyanga, ambapo viongozi hao wa jumuiya wamekutana na wafanyabiashara na kuwataka kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi bora kupitia CCM katika ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani ifikapo Oktoba 29, 2025.

Ujumbe wa viongozi hao kutoka makao makuu ya Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa umejumuisha Mkuu wa Idara ya Uchumi, Mipango na Fedha Jamali Adam, Katibu Msaidizi Idara ya Utawala Eva Jeremiah, na Katibu Msaidizi Idara ya Siasa na Uenezi Nanyaro Urassa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga, Mzee Fue Mrindoko, pamoja na Katibu wa Jumuiya hiyo, Bi. Doris Kibabi.

Akizungumza katika mkutano huo, Jamali Adam amewahimiza wafanyabiashara wa soko la Kambarage kuendelea kuwa wazalendo, kulinda amani na utulivu wa nchi, huku wakijivunia maendeleo makubwa yaliyoletwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Amani ni tunu ambayo kila Mtanzania anapaswa kuilinda. Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa katika kuimarisha uchumi, kuboresha huduma za kijamii na kuwakwamua wananchi kiuchumi. Ni wajibu wetu kushiriki uchaguzi huu kwa amani na kuichagua tena CCM ili maendeleo haya yaendelee,” amesema Jamali.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi Idara ya Siasa na Uenezi Nanyaro Urassa amewasisitiza wafanyabiashara kupuuza watu wanaopotosha au kujaribu kuleta mgawanyiko katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, akisisitiza kwamba Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye dira na uongozi unaojali wananchi.

“Tusikubali kurudishwa nyuma na maneno ya siasa yasiyo na tija. Kura yako ina thamani kubwa, hakikisha unapiga kura kwa CCM ili kuendelea kupata maendeleo,” amesema Urassa.

Naye Eva Jeremiah amewaomba wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu siku ya uchaguzi na kuhamasisha ndugu na marafiki zao kujitokeza kwa wingi.

“Tarehe 29 Oktoba ni siku muhimu. Twendeni kwa amani, tupige kura kumchagua Rais Samia, wabunge na madiwani wote wa CCM. Kila kura ni sauti ya maendeleo,” amesema Eva.

Aidha, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga, Mzee Fue Mrindoko, pamoja na Katibu Bi. Doris Kibabi, wametumia nafasi hiyo kuwaombea kura wagombea wa CCM, wakiwemo Rais Samia, mbunge wa Shinyanga Mjini na mgombea udiwani wa Kata ya Kambarage, Hamis Haji Kabuta, wakisisitiza kuwa ni viongozi wenye nia njema ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Hamis Haji Kabuta, mgombea udiwani wa Kata ya Kambarage kupitia CCM, ameahidi kwamba endapo atachaguliwa, ataboresha miundombinu ya soko la Kambarage na maeneo ya biashara ili wafanyabiashara wafanye kazi katika mazingira salama na ya usafi.

“Kipaumbele changu ni kuhakikisha soko la Kambarage linakuwa la kisasa, lenye miundombinu bora na huduma za msingi zinazostahili. Huu ni muda wa kuleta mageuzi ya kweli ya kimaendeleo,” amesema Kabuta.

Wafanyabiashara wa soko hilo kwa upande wao wamepongeza ujio wa viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na kuahidi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura, huku wakiahidi kuunga mkono wagombea wa CCM katika ngazi zote.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, baadhi ya wafanyabiashara wameeleza kuwa wana imani kubwa na Serikali ya CCM kwa namna inavyotekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo kuboresha huduma za jamii na mazingira ya biashara.

Jumuiya ya wazazi CCM kupitia viongozi wake leo wamezungumza na wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wauzaji wa matunda, mama lishe, wauzaji wa kuku na nyama, mafundi seremala pamoja na waendesha bodaboda ambapo Jana, msafara huo umetembelea Kata ya Chibe, Mjini, na kufanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Ibinzamata.

Ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa inaendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki kwa amani katika uchaguzi mkuu ujao, kudumisha uzalendo, na kuendelea kuiamini CCM kama chama kinacholeta maendeleo ya kweli kwa Watanzania.

Viongozi wa jumuiya ya Wazazi kutoka Taifa wakisaili kwenye kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika ofisi ya CCM kata ya Kambarage.



 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post