" BENKI YA CRDB YAWAKUMBUSHA WATEJA KUENDELEA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZAKE SALAMA NA ZA HARAKA

BENKI YA CRDB YAWAKUMBUSHA WATEJA KUENDELEA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZAKE SALAMA NA ZA HARAKA

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Geita na Tabora, Jumanne Wambura Wagana, amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuwasikiliza wateja ili kujua maeneo yanayohitaji kuboreshwa.

“Tumewakutanisha kwa lengo kuu la kuwasikiliza, kama ilivyo kauli mbiu yetu kwamba CRDB ni benki inayomsikiliza mteja. Tumewaalika ninyi wachache kama wawakilishi wa wengine ili mtupatie maoni yenu, ikiwemo changamoto mnazokutana nazo, mtuambie wapi tuboreshe,” amesema Wagana.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wateja kwa changamoto zilizojitokeza wakati benki hiyo ilipokuwa inafanya mabadiliko ya mfumo ndani ya wiki tatu zilizopita, hali iliyosababisha baadhi ya huduma kusimama au kuchelewa kupatikana.

“Tulifanya mabadiliko kutoka mfumo wa zamani kwenda mpya. Mfumo huu kwa sasa umeunganishwa kimataifa, hata ukienda nchi jirani ikiwemo Burundi unaweza kufanya miamala bila shida. Tumeimarisha sana usalama na kasi ya mifumo yetu ili huduma zetu ziwe za kidijitali, haraka na salama,” amesema Wagana.

Wagana amewashukuru wateja kwa kuendelea kuiamini CRDB na kuichagua kama benki yao ya kudumu, huku akibainisha kuwa CRDB imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wateja kwa uvumilivu na weledi, hususan katika masuala ya mikopo na huduma za kifedha kwa biashara.

Baadhi ya wateja wameipongeza Benki hiyo kwa maboresho ya mifumo na huduma, wakisema changamoto zilizokuwepo awali zimepungua kwa kiasi kikubwa na sasa wanafurahia huduma bora na za uhakika.

Kwa upande wake Meneja wa CRDB Tawi la Shinyanga, Luther Mneney, amesema benki hiyo itaendelea kuwasikiliza wateja na kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa.

“Tumepokea pongezi na maoni yenu. CRDB itaendelea kuboresha huduma kulingana na maoni ya wateja, kwa sababu ninyi ndicho kiini cha mafanikio ya benki yetu,” amesema Mneney.

Hafla hiyo imetamatishwa kwa majadiliano ya wazi ambapo wateja waliuliza maswali, kutoa ushauri na kueleza namna CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono shughuli zao za kiuchumi.

Meneja wa CRDB kutoka matawi ya Tinde, Maganzo na Shinyanga wametoa salamu zao kwa wateja wakati wa mkutano huo, wakisisitiza dhamira ya benki kuendelea kuboresha huduma na kusikiliza mahitaji ya kila mteja.

Wametumia nafasi hiyo kusema wanafarijika kuona wateja wanaendelea kuiamini CRDB na kutumia huduma zake za kibenki, huku wakiahidi kuongeza ubunifu, ukaribu na ufanisi katika kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.

Vilevile wamewashukuru wateja kwa ushirikiano wao na kuwaomba waendelee kuitumia CRDB kama benki salama, ya kisasa na yenye kuthamini mteja katika kila hatua ya safari yake ya kifedha.




Post a Comment

Previous Post Next Post