
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tarime Rorya limemkamata raia mmoja wa Marekani anayedaiwa kuwa mwanajeshi wa Jeshi la Marekani, baada ya kupatikana akiingia nchini na mabomu manne ya kutupwa kwa mkono.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime Rorya leo, Jumatatu, Novemba 16, 2025, tukio hilo lilitokea majira ya saa 06:00 mchana katika eneo la mpaka kati ya Tanzania na Kenya.
Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Charles Onkuri Ongeta, mwenye umri wa miaka 30, mwenye uraia pacha wa Marekani na Kenya, alikamatwa akiwa na mabomu aina ya CS M68. Taarifa hiyo inabainisha kuwa Bw. Ongeta anadaiwa kuwa Sajenti katika Jeshi la Marekani.
Alipokamatwa, Bw. Ongeta alikuwa akitokea Kenya kuingia Tanzania akiendesha gari aina ya Toyota Landcruiser, namba za usajili KDP 502 Y.
Kamanda wa Polisi amesisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Umiliki wa Silaha, Bw. Ongeta hakuwa na kibali cha kuingia na silaha hizo nchini, na hata kama angeomba, asingepewa.
"Ushahidi unaendelea kukusanywa sambamba na kuhojiwa ... ili hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake," ilisema taarifa hiyo.
Post a Comment