" RAIS SAMIA AKERWA NA VURUGU, ATOA AGIZO KWA VYOMBO VYA ULINZI

RAIS SAMIA AKERWA NA VURUGU, ATOA AGIZO KWA VYOMBO VYA ULINZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelaani vikali matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika baadhi ya miji nchini, huku akitaja madhara mabaya ya vitendo hivyo na kutoa onyo kali kwa wachochezi.

Katika hotuba yake ya kuapishwa, Mhe. Rais alieleza kusikitishwa na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, akibainisha athari zake:

Rais Samia alifafanua kwamba matukio hayo hayakwenda sambamba na taswira na sifa za Tanzania kwani  matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza kwenye baadhi ya Majiji na Miji, yamesababisha upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za Umma na mali za Watu binafsi. 

Alitoa onyo kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa amani, akitaka watambue kuwa vurugu huishia kupimana nguvu, ila mazungumzo huzaa mshikamano. Aliwaasa Watanzania kuchagua hekima badala ya ghadhabu, upendo badala ya chuki, na amani badala ya vurugu.

"Niwasihi Watanzania tuchague hekima badala ya ghadhabu; amani badala ya vurugu... Usalama wa Taifa lolote hulindwa na wote kwa nguvu na gharama zozote".

Kama hatua ya haraka, Rais Samia alitoa maagizo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,kuendelea kufuatilia na kuchunguza kwa undani zaidi kilichotokea, huku akitaka nchi irudi katika hali yake ya kawaida kwa haraka.

Zaidi ya hayo, Kamati ya Ulinzi ya Kitaifa, pamoja na Kamati za Ulinzi za Mikoa na Wilaya, zimeagizwa kuhakikisha kwamba maisha ya Wananchi yanarejea mara moja kuanzia leo.

Mhe. Rais alishukuru wagombea wengine 17 wa nafasi ya Urais kwa kuonesha ukomavu wa kidemokrasia kwa kushindana kwa hoja, na kudhihirisha kuwa siasa sio vita.

Alikumbusha kwamba, kwa mujibu wa falsafa ya 4R's, lengo la Serikali ni kuunganisha Taifa kupitia kuzungumza na kuelewana (Reconciliation). Aliahidi kuwa Serikali itakuwa na nguvu zaidi pale kila sauti, chanya na hasi, zinaposikilizwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Mhe. Rais ameeleza kuwa masuala ya kina kuhusu mwelekeo wa kazi za Serikali kwa kipindi kijacho, na ufafanuzi wa dhana ya Kazi na Utu, utatolewa katika Hotuba ya Uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Post a Comment

Previous Post Next Post