Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza rasmi kuendelea kwa kawaida kwa sekta ya utalii kutokana na kurejea kwa hali ya amani na utulivu baada ya kudhibitiwa kwa vurugu zilizotokea kati ya Oktoba 29 na Novemba 1, 2025.
Katika taarifa rasmi ya usafiri (Travel Advisory) iliyotolewa Novemba 4, 2025, na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ntengenjwa Hosseah, Wizara imehakikishia umma, wadau na wageni kuwa shughuli za utalii katika maeneo mbalimbali ya nchi zinaendelea bila vikwazo.
"Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuufahamisha umma, wageni na wadau wa Sekta ya Utalii ndani na nje ya nchi, kwamba hali ya amani na utulivu imerejea na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinaendelea baada ya kudhibitiwa kwa vurugu zilizozuka kati ya tarehe 29 Oktoba hadi 1 Novemba, 2025," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Tanzania, kama Mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), inatekeleza kikamilifu majukumu yake ya kuhakikisha usalama wa wageni wote, wa ndani na nje.
Huduma za Usafiri: Vituko vyote vya kuingia na kutoka nchini ikiwemo usafiri wa anga, barabara, reli, meli, na sambamba na usafiri wa umma, vinaendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa kawaida.
Shughuli za Utalii: Shughuli zote za utalii na huduma kwa wageni zinaendelea kutolewa katika maeneo yote nchini.
Wito kwa Wasafiri: Wasafiri wamehimizwa kuendelea na mipango yao ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania bila hofu yoyote.
Wizara imesisitiza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, yenye utulivu, na mazingira rafiki kwa shughuli zote na kwamba Serikali inachukua hatua zote za kiusalama kuhakikisha wageni wote wanabaki salama wakati wote wa safari yao.

Post a Comment