" MKUU WA MKOA KAGERA APONGEZA UZALENDO WA WANANCHI, AWATAKA KUENDELEZA AMANI, AFUNGUA TAMASHA LA IJUKA OMUKA 2025

MKUU WA MKOA KAGERA APONGEZA UZALENDO WA WANANCHI, AWATAKA KUENDELEZA AMANI, AFUNGUA TAMASHA LA IJUKA OMUKA 2025

‎Na Fabius Clavery, Misalaba Media - Kagera.‎Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatuma Mwassa, amewashukuru wananchi wa mkoa huo kwa kuendelea kulinda heshima ya Kagera pamoja na Taifa kwa ujumla, hasa katika kipindi cha Uchaguzi na baada ya uchaguzi, kwa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu na kutojihusisha kwa namna yoyote katika matukio ya uvunjifu wa amani.‎Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo Desemba 18, 2025, wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Ijuka Omuka 2025, linaloandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa sambamba na Dua na Sala ya Kuliombea Taifa.‎Aidha, amewaomba wananchi wa Kagera kuendelea kuwa mfano kwa Watanzania wengine katika suala la kutunza amani.‎“Niwashukuru sana wana Kagera; mlionesha uzalendo wa kutosha katika kipindi chote tulichopita kama Taifa. Wana Kagera hamkushiriki katika uvunjifu wa amani kwa namna yoyote,” alisema Mkuu wa Mkoa.‎Aliongeza kuwa wananchi wa Kagera wanapaswa kuendelea kuwafundisha Watanzania wengine umuhimu wa kulinda amani, akibainisha kuwa mkoa huo umewahi kupitia nyakati ngumu katika historia yake.‎“Kagera ilishapitia nyakati ngumu kama Vita ya Kagera ya mwaka 1978, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, kuzama kwa Meli ya MV Bukoba, tetemeko la ardhi pamoja na ajali ya ndege. Haya yote ni majonzi makubwa, hivyo hatuombi yajitokeze tena hapa,” alisisitiza.‎Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Tamasha la Ijuka Omuka 2025 litajumuisha kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Kagera ili kuchochea maendeleo, Bonanza la Michezo, pamoja na kuenzi utamaduni wa mkoa huo ikiwemo vyakula vya asili.‎Mapema, akitoa salamu kwa niaba ya viongozi wa dini, Askofu Ayubu Silivester, Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste Mkoa wa Kagera (CPCT), aliwaomba wasomi, wataalamu na wawekezaji kuikumbuka Kagera kama nyumbani na kuendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuendeleza mkoa huo katika nyanja zote.‎Tamasha la Ijuka Omuka 2025 limeanza rasmi Desemba 18, 2025, mjini Bukoba mkoani Kagera, na linatarajiwa kuhitimishwa Jumapili, Desemba 21, 2025, likiwa na kaulimbiu isemayo:‎“IJUKA OMUKA – WEKEZA KAGERA, IRUDISHE KATIKA UBORA WAKE (Make Kagera Great Again).”

 

Post a Comment

Previous Post Next Post