" MWANAMKE AFARIKI, WATANO WANUSURIKA BAADA YA NYUMBA KUUNGUA MOTO SHINYANGA

MWANAMKE AFARIKI, WATANO WANUSURIKA BAADA YA NYUMBA KUUNGUA MOTO SHINYANGA

Mwanamke mmoja aitwaye Agnes James anayekadiliwa kuwa na umri wa Miaka 33 amefariki Dunia huku watu wengine watano wa familia hiyo wakinusurika kifo baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuungua kwa moto katika eneo la Mwasele B, Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza na Misalaba Media, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwasele B, Cosmas Lukas, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa amepata taarifa majira ya saa tisa usiku wa kuamkia leo Desemba 16, 2025 ambapo chanzo cha moto huo kinadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme, ingawa bado hakijathibitishwa rasmi.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa moto huo ulianzia sebuleni, ambapo wanafamilia waliokuwemo ndani ya nyumba hiyo walihisi hewa kuwa nzito, hali iliyowafanya kujaribu kutoka nje na kwamba baada ya kushindwa kufungua mlango, walitoa sauti kuomba msaada na majirani walifanikiwa kuwafungulia.

Inadaiwa kuwa marehemu Agnes James alirudi ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuchukua fedha zake, ndipo moto ulimzidi nguvu na kusababisha kifo chake.

Aidha, Cosmas Lukas ameeleza kuwa Vicent Jacobo ni mjasiriamali, na vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya nyumba hiyo vimeteketea kwa moto, ikiwemo biashara yake ya kuku, ambapo kuku mmoja pekee ndiye aliyeokolewa. Vitu vingine vilivyoteketea ni pamoja na vitanda, vyakula, viriji pamoja na mali nyingine mbalimbali za thamani.

Mwenyekiti wa mtaa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto na kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa haraka pindi majanga yanapotokea.

Afisa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Edward Seleman, amesema walipopata taarifa na kufika eneo la tukio walikuta moto ukiwa umeshika kasi kubwa, huku mwanamke huyo tayari akiwa amefariki dunia ndani ya nyumba akiwa ameshika fedha mkononi.

“Tukio lilitokea majira ya saa 9 usiku. Tulipata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwasele B na kufika eneo la tukio, tukafanikiwa kuuzima moto, lakini Mama mwenye nyumba tulimkuta tayari ameshafariki,” amesema Seleman.

Ameeleza kuwa awali marehemu alikuwa ameokolewa pamoja na familia nzima na mume wake na wote walikuwa nje ya nyumba. Hata hivyo, marehemu alirudi tena ndani kwa ajili ya kufuata fedha zake, ambazo inadaiwa alizipata baada ya kuvunja kikundi cha vikoba, kiasi ambacho bado hakijajulikana, ndipo moto ukamzidi na kusababisha kifo chake.

Seleman amesema baada ya uchunguzi wa awali, chanzo cha moto huo kimebainika kuwa ni hitilafu ya umeme. Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kuhakikisha mifumo ya umeme, hususan katika nyumba za zamani, inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili kuepuka majanga kama hayo.

Nao baadhi ya majirani wa marehemu, akiwamo David Jonson, wamesema walijaribu kuuzima moto huo mara walipofika eneo la tukio, lakini walishindwa kutokana na ukali wa moto na ukosefu wa vifaa stahiki, hali iliyosababisha kushindwa kumuokoa Mama mwenye nyumba.

 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post