" NIDHAMU, MAARIFA NA MOYO WA KUJITOLEA HUUNDA KIONGOZI WA KESHO

NIDHAMU, MAARIFA NA MOYO WA KUJITOLEA HUUNDA KIONGOZI WA KESHO

Kuna vigezo vitatu muhimu vinavyojenga kiongozi bora wa kijana: Nidhamu, Maarifa, na Moyo wa Kujitolea. 

Haya yanaonekana  kwenye mitandao katika majadiliano yanayogusa maisha ya vijana ambao hawataki kuendekeza uchochezi na kuharibu taifa lao.

Kwa mujibu wa ujumbe uliopo kwenye mitandao, sifa hizi tatu huunda kijana anayeheshimika, anayesikilizwa, na anayeweza kuaminika kuliongoza taifa huko mbeleni.

Ujumbe huu unafika wakati ambapo Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Ofisi ya Rais inayosimamia Maendeleo ya Vijana, inaweka mikakati thabiti ya kuwawezesha vijana.

Hatua za Serikali za kuwezesha vijana zimethibitishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka. Waziri Nanauka alieleza dhamira ya Serikali katika kuboresha Vituo vya Maendeleo ya Vijana ili viwe chachu ya kuwawezesha vijana kiuchumi, kijamii na kielimu.

Vituo vikuu vitatu vilivyotajwa na Waziri ni Sasanda (Songwe), Ilonga (Morogoro), na Marangu (Kilimanjaro).

Alikiri kuwa baadhi ya vituo, kama Sasanda, vilikoma kutoa mafunzo kwa muda mrefu (tangu 2008), lakini Serikali sasa imejipanga kuviboresha na kuvitumia kikamilifu ili kuwasaidia vijana katika maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa vituo hivi vina manufaa makubwa kwa vijana katika kuwajengea ujuzi wa vitendo, ambao ni muhimu katika soko la ajira.

Waziri Nanauka alikumbusha kwamba Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa kwa vijana, kiasi cha kuunda Wizara maalum kushughulikia masuala yao.

Hivyo, vijana wanahimizwa kutambua na kufuatilia kwa karibu mipango hii ya Serikali. Kwa kutumia vituo hivi, vijana wanaweza kupata ujuzi unaohitajika, kuanzisha miradi yao wenyewe, na hivyo kutengeneza fursa za ajira kwao na kwa wengine.

Dkt. Kedmon Mapana, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana, naye alisisitiza umuhimu wa watendaji kutembelea vijana, kufanya kazi kwa kasi, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kutekeleza shughuli za vijana.

Hii inamaanisha vijana wanatakiwa kujifunza, kujiendeleza, na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali huku wakidumisha sifa za uadilifu ili kuwa tayari kuongoza taifa kwa heshima na uwezo kesho.

Post a Comment

Previous Post Next Post