" TRA KAGERA YAJIPANGA KUWEZESHA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI KULIPA KODI KWA HIARI

TRA KAGERA YAJIPANGA KUWEZESHA WAFANYABIASHARA NA WAWEKEZAJI KULIPA KODI KWA HIARI

Na Fabius Clavery, Misalaba Media -Kagera.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imeeleza kuwa imejipanga kutoa ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji mkoani humo, kwa lengo la kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kulipa kodi zinazostahiki kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Bw. Castro John, wakati akizungumza na Misalaba Media pembezoni mwa kikao cha Baraza la Wafanyabiashara kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Desemba 18,2025.

Meneja huyo amesema kuwa kwa sasa TRA inaendelea kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Kagera wanapata elimu na taarifa sahihi za kikodi, hatua itakayowasaidia kulipa kodi zao kwa hiari na kwa usahihi, sambamba na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

“Tunahakikisha tunatoa elimu kwa wafanyabiashara kwa sababu wengine hawakuwa na uelewa wa masuala ya kodi. Unakuta mtu anaingiza bidhaa, kwa mfano kutoka Uganda, ambazo kisheria hazihitaji kulipiwa kodi, lakini kutokana na kukosa elimu analazimika kutumia njia zisizo rasmi. Sisi tunawawezesha kwa kuwapatia elimu, lakini pia kiuchumi, kwani mfanyabiashara anapopata Tax Clearance inamwezesha kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha,” amesema Bw. Castro.

Aidha, ameongeza kuwa Jukwaa la Ijuka Omuka limechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya walipakodi wapya mkoani Kagera, kutokana na elimu na huduma zilizotolewa wakati wa jukwaa hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post