" WAKULIMA WA KOROSHO TUNDURU WALIPWA ZAIDI YA SH. BILIONI 92.4

WAKULIMA WA KOROSHO TUNDURU WALIPWA ZAIDI YA SH. BILIONI 92.4






Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja,akizungumza na wawakilishi wa wakulima na viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)na Chama Kikuu cha Ushirika(TAMCU) baada ya kufanyika kwa mnada wa tano wa zao la korosho,katikati Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule na kulia Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Milongo Sanga.Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Shauri Mokiwa akizungumza kwenye mnada wa tano wa zao la korosho.

‎Na Mwandishi Wetu,Tunduru

‎WAKULIMA wa zao la korosho wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru(TAMCU)wamelipwa zaidi ya Sh. bilioni 92.416 baada ya kuuza jumla ya kilo 36,994,519 kwenye minada mitano kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

‎Kaimu Meneja wa TAMCU Zainabu Sendema alisema,katika mnada wa 1 hadi 4 wakulima wameuza kilo 31,272,958 zenye thamani ya Sh.78,026,310,000 na katika mnada wa tano kilo 5,721,561 zenye thamani ya Sh.14,389,725,913 zimeuzwa huku bei wastani ni Sh.2,515 kwa kilo moja.

‎Sendema alisema,katika minada yote 1 hadi 5 bei wastani ni Sh.2,560 na bei ya chini 2,420 ambayo imewezesha wakulima kupata fedha nyingi kutokana na kilimo cha zao hilo.‎

‎Sendema,amewataka wakulima kuhakikisha wanalinda bei nzuri inayotolewa na wanunuzi katika msimu huu 2025/2026 kwa kupeleka korosho zenye ubora kwenye maghala ya vyama vya msingi vya Ushirika na Chama Kikuu kwa ajili ya kupata bei nzuri.

‎“Kwa ujumla katika minada yote iliyofanyika bei nzuri,nawaomba wakulima wetu wahakikishe wanazingatia kanuni za uandaaji korosho ikiwemo kukauka vizuri na kuhifadhi sehemu sahihi kabla ya kupeleka kwenye mnada ili waweze kuendelea kunufaika na bei zinazotolewa na wanunuzi”alisena Sendema.

‎Mwenyekiti wa Chama hicho Mussa Manjaule alisema,katika mnada wa tano walijitokeza wanunuzi 16 wamenunua korosho zote zilizoingizwa kwenye maghala mbalimbali huku bei ya chini ikiwa Sh.2,420,bei ya juu 2,550 na bei wastani 2,515.

‎Manjaule,amewashukuru wakulima kukubali kuuza korosho zao katika mnada wa tano huku akiwapongeza kutokana na jitihada kubwa wanazofanya katika uzalishaji wa zao hilo na mazao mengine yanayosimamiwa na TAMCU.‎

‎Alisema,awali walikuwa na mashaka juu ya uzalishaji katika msimu 2025/2026,lakini hadi kufikia mnada wa tano wamefanikiwa kuzalisha tani 36,000 kati ya lengo la kuzalisha tani 35,000.‎

‎“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,malengo yetu katika msimu huu ilikuwa kuzalisha tani 35,000 lakini hadi kufikia mnada huu wa tano tayari tumevuka lengo kwa kuzalisha na kukusanya zaidi ya tani 36,tunaamini tutafikisha hadi tani 40,000,hizi ni jitihada kubwa za wakulima na wadau wengine wa tasinia ya korosho ikiwemo bodi ya Tamcu”alisema Manjaule.‎

‎Aidha alisema,Tamcu itajitahidi kulipa fedha za wakulima kwa wakati ili kuwa mfano kwa vyama vingine vinavyojihusisha na zao la korosho na kuwaondolea wakulima usumbufu kutoka vijiji kuja mjini kuulizia malipo yao.‎

‎“Tamcu ndiyo Chama pekee ambacho kinajitahidi sana kulipa wakulima kwa wakati,wewe mwenyewe ni shahidi baadhi ya maeneo suala la malipo ya fedha za wakulima ni changamoto kubwa tofauti na sisi,kwa umoja wetu kati ya Amcos na Chama kikuu tumejipanga kuwa mshindi wa kwanza hapa nchini kulipa wakulima wetu kwa wakati”alisema.

‎Manjaule,amewataka wakulima kuanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo cha korosho kwa kukwatua mashamba yao na kupanda mazao mengine madogo madogo yatakayowaingizia kipato badala ya kusubiri hadi msimu wa korosho.

‎Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja,ameupongeza uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika(TAMCU) na bodi ya korosho Tanzania kwa kuendesha minada yake kwa uwazi na wakulima kuzalisha korosho zenye ubora mkubwa.

‎Alisema,tangu mnada wa kwanza ulipofunguliwa hadi sasa wakulima wa Wilaya hiyo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla,wameuza korosho zenye ubora na hakuna zilizokataliwa na wanunuzi kwa kuwa chini ya kiwango.‎

‎Amewasisitiza wakulima,kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa kilimo kupitia bodi ya Korosho Tanzania na waendelee kuzingatia ubora unaoanza kwenye maandalizi shambani hadi pale wanapokusanya kabla ya kupeleka kwenye maghala.

‎Masanja,ameiagiza Tamcu kuhakikisha wanalipa fedha za wakulima kwa wakati na watunza maghala wanaondoa korosho za minada iliyotangulia kwenye mgahala yao ili kuepuka changamoto inayoweza kutokea.

‎Naye Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Shauri Mokiwa,amewakumbusha wakulima kuendelea kutunza mashamba yao kwa kukwatua ili kuwezesha maji kuingia kirahisi chini kwenye mizizi.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post