" HII NDIYO SABABU YA CHAMA KURUDI SIMBA

HII NDIYO SABABU YA CHAMA KURUDI SIMBA

 

Dar es Salaam. Siku chache zimepita baada ya kiungo mshambuliaji, Clatous Chota Chama kurejea kwenye Klabu yake ya zamani ya Simba akitokea Singida Black Stars. Chama alijiunga na Singida BS kwenye dirisha kubwa la usajili akitokea Yanga na ameitumikia timu hiyo kwa nusu msimu pekee.
Katika kipindi hicho cha nusu msimu alichodumu kwa walima Alizeti hao, Chama aliisaidia Singida BS kushinda taji la michuano ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame pia aliisaidia kufuzu katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.

KUREJEA MSIMBAZI TENA
Chama amejiunga na Simba ikiwa ni safari ya tatu kufanya hivyo ambapo mara ya kwanza alitua Simba mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, akaondoka Agosti 2021 alipouzwa kwenda RS Berkane ya Morocco ambako hakudumu sana kwa Wamorocco hao, akarejea tena Simba Januari 2022.

Julai 2024, Chama alipomaliza mkataba wa kuitumikia Simba, alisajiliwa na Yanga ambako alipodumu kwa msimu mmoja wa 2024-2025, kisha Septemba 2025 alitua Singida Black Stars, kabla ya kurejea tena Simba Januari 2026.

Uamuzi wa Simba kumrudisha Chama ni baada ya kufanya biashara ya kumuuza Jean Charles Ahoua kwenda CR Belouizdad ya Algeria ambaye alisajiliwa na Simba msimu uliopita 2024-2025 akitokea Klabu ya Stella d’Adjamé ya Ivory Coast akichukua nafasi ya Mwamba wa Lusaka baada ya kutua Yanga.

Kurudi kwa kiungo huyo ndani ya Simba ni wazi kabisa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza bado ipo, hii ni baada ya kuondoka kwa Ahoua ambaye alifanikiwa kujijengea Ufalme ndani ya klabu hiyo msimu wake wa kwanza akifunga mabao 16 na kutoa pasi tisa zilizozaa mabao katika Ligi Kuu Bara huku akitoa mchango wa kuifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2024-2025.

Katika kikosi cha Simba eneo la kiungo mshambuliaji kutokea kati, kabla ya ujio wa Chama, timu hiyo iliundwa na Neo Maema aliyetua kwa mkopo kutoka Mamelodi, Morice Abraham, Jean Ahoua na Awesu Ally Awesu.

Awesu amepelekwa Police Kenya kwa mkopo, Ahoua tayari ameuzwa CR Belouizdad huku wakibaki Maema na Morice pekee ambao walitua kikosini hapo mwanzoni mwa msimu huu.

KINACHOMBEBA
Jambo la kwanza, Chama ni mzuri katika kutengeneza mabao, kwa muda aliokuwa Simba alipiga jumla ya pasi 60 za mwisho akicheza jumla ya mechi 183 za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa.

Katika eneo lake la kiungo mshambuliaji, Chama amekuwa kiungo muhimu kila anapokwenda na kupewa nafasi ya kucheza kwani amehusika kwa kiasi kikubwa wakati Singida Black Stars inafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiziondoa Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1 na Flambeau du Centre ya Burundi kwa jumla ya mabao 4-2.

Kati ya mabao hayo saba yaliyofungwa na Singida Black Stars, Chama amehusika kwenye matatu, akifunga mawili na kutoa pasi moja ya bao.

Jambo la pili, Chama akipata nafasi, anafunga mwenyewe. Ni kazi nyingine ambayo Chama anaiweza vizuri na inaweza kuwa faida kurejea kwake Simba kwani kipindi yupo kikosini hapo katika mechi 183 za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, alifunga mabao 42.

Msimu huu alipokuwa na Singida Black Stars, Chama alifunga mabao sita katika mashindano tofauti ikiwamo matatu ya Kombe la Kagame ambapo aliibuka mfungaji bora.

AMVUTIA KOCHA
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker alishindwa kujizuia kwa kuonyesha kuvutiwa na urejeo wa kiungo huyo fundi raia wa Zambia akisema usajili huo ni hatua muhimu katika kuimarisha kikosi hicho kutokana na uzoefu wake.

“Kurudi kwa Chama ni jambo zuri. Anafahamu Simba, anajua jinsi ya kushirikiana na wachezaji wenzake na ni mchezaji mwenye akili kubwa ya kimchezo naamini ataongeza kitu kwenye timu,” alisema Barker.

Kocha Barker aliongeza, ujio wa Chama unaongeza machaguo zaidi katika eneo la kiungo mshambuliaji baada ya kuondoka kwa Ahoua na ni fursa ya kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

“Chama ni mchezaji ambaye anaweza kuongoza na kuhimiza wengine. Hii inatupa imani ya kuwa tunayo timu yenye nguvu na yenye mpangilio mzuri,” aliongeza Barker.

Barker ameonyesha matarajio makubwa kwa kikosi chake katika maandalizi ya mechi ya marudiano ya kimataifa dhidi ya Esperance De Tunis, licha ya kutofanya vizuri katika mechi ya kwanza ambayo Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 ugenini.

Katika mechi dhidi ya Esperance, Chama alitambulishwa mchezoni katika kipindi cha pili akichukua nafasi ya Morice. Katika mchezo huo Mwamba wa Lusaka alionesha utulivu kwenye eneo la kiungo mshambuliaji licha ya kutoisaidia timu yake kusawazisha bao lililofungwa kipindi cha kwanza na Jack Diarra ambaye alimalizia kwa ustadi pasi ya Ben Hamida.

Simba inaendelea kuburuza mkia katika msimamo wa kundi D ikiwa haina pointi baada ya kupoteza mechi tatu za kwanza. Hata hivyo, bado wananafasi ya kutinga hatua ya mtoano ikiwa watafanya vizuri katika mechi tatu zilizosalia pia kuombea matokeo ya mechi nyingine zitakazohusisha timu za Esperance, Stade Malien na Petro Luanda yawe yenye faida kwa upande wao.

Mbali na matokeo hayo kuiweka rehani ndoto ya Simba kucheza robo fainali, yameifanya pia iandike rekodi mbaya ya kucheza mechi tatu mfululizo za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika bila kupata pointi.

Simba imevunja rekodi yake yenyewe ya msimu wa 2022/2023 ambapo katika mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi, ilipoteza mbili na kushinda moja. Hadi sasa Simba imeruhusu mabao manne katika michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa huku yenyewe ikifunga moja pekee.

Post a Comment

Previous Post Next Post