Na Mapuli Kitina
Misalaba
Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga imeanza rasmi kutoa
huduma za afya za kibingwa ikiwemo huduma za daktari bingwa wa magonjwa ya
wanawake na uzazi kila siku pamoja na kliniki ya daktari bingwa wa mifupa
(Orthopedic) kila Jumamosi, hatua inayolenga kuwasogezea wananchi huduma muhimu
karibu zaidi na kuwasaidia kupunguza gharama walizokuwa wakizitumia kusafiri
hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga iliyopo Mwamwaza.
Akizungumza kuhusu huduma hizo, Mganga Mfawidhi (MOI)
wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Pierina Mwaluko,
amesema ujio wa madaktari bingwa katika hospitali hiyo ni mkombozi mkubwa kwa
wakazi wa Manispaa ya Shinyanga na mkoa kwa ujumla.
“Kwa
muda mrefu wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa
kufuata huduma za kibingwa. Sasa huduma hizo zinapatikana moja kwa moja hapa Manispaa ya Shinyanga,” amesema.
Dkt. Mwaluko ameongeza
kuwa huduma nyingi za kibingwa zilizokuwa zinapatikana Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa Mwawaza sasa zinapatikana Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, jambo
linalosaidia kupunguza msongamano katika hospitali ya rufaa na kuongeza ufanisi
wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Amebainisha kuwa
hospitali imejipanga vyema kuhudumia wagonjwa wa nje na wa ndani, ikiwa na
jengo la OPD lenye miundombinu ya kisasa na wodi ya wanawake iliyoboreshwa kwa
ajili ya huduma za ndani na kwamba hospitali ina vifaa vya kisasa vya uchunguzi,
ikiwemo maabara iliyoimarishwa na huduma za mionzi kama ultrasound,
zinazosaidia kubaini magonjwa haraka na kwa usahihi.
Kwa upande wa huduma za
upasuaji, Dkt. Mwaluko amesema hospitali ina jengo la upasuaji (theatre) lililoandaliwa
kwa viwango vinavyotakiwa, likiwa na chumba cha upasuaji chenye vifaa muhimu
kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo.
Kwa upande wake, Dkt. Elipidius Theodory, Daktari Bingwa wa Uzazi na
Magonjwa ya Wanawake, amesema hospitali inatoa huduma za uchunguzi na matibabu
ya changamoto mbalimbali za afya ya uzazi kwa akina mama, ikiwemo matatizo ya
mfumo wa uzazi, huduma za uchunguzi wa saratani, uzazi wa mpango pamoja na
ufuatiliaji wa wajawazito, wakiwemo wenye mimba hatarishi.
Uongozi wa Hospitali ya
Manispaa ya Shinyanga umehitimisha kwa kuwakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa
Shinyanga na mikoa ya jirani kufika hospitalini hapo kupata huduma za kibingwa,
ukisisitiza kuwa sasa huduma hizo zinapatikana karibu,
kwa ubora na kwa gharama nafuu.
Mganga Mfawidha wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga Dkt. Pierina Mwaluko, akizungumza na Misalaba Media.

Daktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga Dkt. Elipidius Theodory, akizungumza.






Post a Comment